Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na
mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu (Oktoba
9, 2023) katika Ofisi ndogo za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam,
Waziri Jafo alipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko
la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa
katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa
mashirika hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa
Mazingira wa Dunia – GEF, uliofanyika katika Mji wa
Vancouver nchini
Canada ambapo ambapo nchi
zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa
mazingira duniani.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Tanzania bado ina
mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa
mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu
kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia
nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa
miradi hiyo.
“Tanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi.
Leo ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji
wanavyohangaika na mifugo ya….Si hapo tu na Mpwapwa napo hali nayo si
nzuri…Hivyo tunahitaji miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru
jamii zetu” amesema Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya
Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali
ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji
ili kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Akitolea mfano Dkt. Muyungi
amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mradi
ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi
katika maeneo ya barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa
udongo baharini.
Dkt. Muyungi amesema
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya
kimataifa ili juhudi za pamoja ziendelee kuimarishwa katika kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi ya uhifadhi na
usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa katika jamii.
Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika hayo
wameihakikishia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa maandalizi muhimu
ya uwasilishaji wa taarifa za vipaumbele vya miradi ya mazingira inayosimamiwa
na GEF imekamilika na kwa pamoja wameishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea
kufanya katika kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya amesema Shirika
hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha juhudi
za pamoja zinaendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabia nchi ikiwemo ufadhili wa miradi na uwezeshaji wa fedha.
“Katika andiko letu UNEP tutakalowasilisha GEF
tumeainisha maeneo mapya ya miradi kwa Tanzania…Tayari tuna miradi katika
maeneo matano…Tumepanga kuangalia awamu ijayo tuanze kuitekeleza Zanzibar na
maeneo ya Mikoa ya Nyanda za Juu kusini” amesema Bi. Makenya.
Mashirika yahudhuria kikao hicho kilichoitishwa Mhe. Waziri Jafo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambapo mashirika hayo yanafadhili miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Miradi inayofadhiliwa na mashirika hayo ni pamoja na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS).
No comments:
Post a Comment