Habari za Punde

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Awataka Wasanii Kukemea Maovu Kupitia Tungo Zao

Waziri wa Maendeleo ya  Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Riziki  Pembe Juma akikata utepe kuashiria uzinduzi wa CD ya Tungo njema wakati wa hafla ya siku ya Tungo njema iliyoandaliwa na uongozi wa Redi Al-nour na kufanyika  katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein Wilaya ya Mjini Unguja.

Waziri wa Maendeleo ya  Jamii ,Jinsia , Wazee  na Watoto Mhe. Riziki  Pembe Juma akizunguma na Wadau wa Sanaa za Mashairi kuhusiana na umuhimu wa kuelimisha jamii kupitia sanaa hiyo huko Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein Mjini Unguja.

PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa,     Maelezo

Waziri wa  Maendeleo ya  Jamii ,Jinsia , Wazee, na Watoto, Mhe Riziki Pembe Juma amewataka wasanii wa tungo za mashairi  kujikita katika kutunga tungo zenye kukemea maovu yaliomo katika jamii.

Akizungumza na watunzi,waghani na wapenzi wa mashairi katika hafla ya siku ya tungo njema iliyofanyika  Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein amesema kufanya hivyo kutapunguza vitendo viovu kwani jamii ya walio wengi hufuatilia sanaa za mashairi ikiwemo tenzi na mashairi.

Alisisitiza kuwa kila mmoja ana jukumu la kukemea mambo maovu kwa namna moja au nyengine hivyo aliwataka wasanii kupitia tungo zao kujikita katika kuzungumiza maadili ya mzanzibar na kurekebisha pale ambapo maadili hayo yanapoporomoka.

 Alisema ujumbe unaotolewa kupitia tungo hizo huifikia jamii  kwa haraka zaidi   hivyo aliwataka wasanii wa sanaa hiyo kushirikiana na Serikali katika kupinga vitendo vya udhalilisha kwani vinaonekana kuendelea kushamiri siku hadi siku.

Mhe Riziki alifahamisha kuwa udhalilishaji sio kubakwa tu hata kutamkiwa maneno yasiofaa ni udhalilishaji,hivyo aliwataka watunzi  wa tungo njema kutumia elimu, ubunifu na ujuzi wao katika kukemea vitendo hivyo visitokee hasa kwa wanawake,mayatima  na wenye mahitaji maalum.

Hata hivyo   aliupongeza  uongozi wa Redio Al-nour  kwa kuandaa siku hiyo muhimu iliyowashirikisha watu tofauti ikiwemo mayatima na wenye mahitaji maalum.

Awali Mhe. Riziki alichukua fursa hiyo kuitaka jamii kuuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Huseein Ali Mwinyi  katika kuwaletea maendeleo wananchi wake nakuwataka kuendelea kudumisha amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo zaidi .

Mkurugenzi Baraza la KiswahiIi Zanzibar Dkt.Mwanahija Ali Juma  amesema  BAKIZA itaendelea kuunga mkono juhudi za wasanii wa mashairi  kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuiendeleza na kuikuza lugha hiyo.

Amesema wasanii hao ni kundi ambalo halipaswi kuachwa nyuma kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia kuelimisha na kuikosoa jamii  juu ya mambo mbalimbali yanayotokezea Nchini.

“Mashairi hayo hutolewa kwa Kiswahili na hupokelewa na hadhira mbalimbali ndani na nje ya Nchi hiyo ni njia moja ya kukisambaza kiswahili,hivyo ipo haja kukuza na kuendeleza vipaji vyao ili sanaa hiyo iendelee kutumika siku hadi siku”alifahamisha Dkt.Mwanahija

Akisoma Risala ya washairi Omar Khamis  amesema Dhamira kuu ya tungo njema ni kukemea ,kushajihisha,kukosoa na kuelemisha juu ya mambo mbalimbali  yanayotokea katika jamii.

Aidha alisema kupitia tungo za mashairi wamefanikiwa kuchochea  maendeleo katika jami kwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari , kupinga vitendo vya udhalilishaji, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza amani  pamoja na kujenga mahusiano mazuri ya Taasisi za Serikali na  Binafsi

Awali alifahamisha kuwa madhumuni ya siku ya tungo njema ni kutambua na kuthamini juhudi na  mchango wa wasanii wa mashairi na tenzi  katika kujenga jamii iliyobora

Maadhimisho hayo ni ya pili kufanyika ambapo  kwa mwaka yameshirikisha wadau mbali mbali wa Tungo njema,Watoto yatima na watu wenye mahitaji maalum.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.