Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amewataka Wahitimu wa Vyuo Vikuu Kutumia Elimu Zao Kuchangia Maendeleo ya Nchi

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wahitimu wa vyuo vikuu kutumia elimu zao, kuchangia Maendeleo ya nchi kwa nafasi mbalimbali za taaluma zao.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo, kwenye mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, Unguja.

Alisema, Elimu ni ajenda muhimu kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2020 - 2025, yenye lengo la kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa na wananchi wake.

Alisema nguvu kazi yenye elimu bora na maarifa ina mchango muhimu kwa maendeleo ya kila sekta.

Halkadhalika, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane imejikita zaidi kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu ikiwa ni kipaombele chake, kwa kuzifanyia kazi changamoto zinazotokana na sekta hiyo ikiwemo kuboresha maendeleo na miundombinu ya kisasa, kuimarisha vifaa vya kufundishia, maabara, maktaba, vyumba vya kompya, vyoo na mazingira mazuri ya walimu katika kuchochea mageuzi na maendeleo ya kiuchumi wa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza, uhusuano na ushirikiano uliopo baina ya   Serkali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Taasisi ya elimu ya juu vikiwemo vyuo vikuu ya umma na binafsi, vina mchango muhimu kuhakikisha Zanzibar inatoa elimu bora na kuchochea maendeleo kwa kada zote.

Alieleza vyuo vikuu na taasisi nyengine za elimu Zanzibar, vinafanya kazi nzuri ya kuwaandaa wataalamu wakushika nafasi mbalimbali za utumishi Serikalini  na taasisi binafsi.

Akizuzungumzia maendeleo kwenye Sekta ya Afya, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali pia imeweka mkazo zaidi kuimaisha miundominu ya kisasa kwenye hospitali zote za Serikali kwa kufanya mageuzi makubwa ikiwemo kuboresha miundominu ya kisasa ya matibabu kwa hospitali zote za Wilaya Unguja na Pemba pamoja na kuangalia upya sera ya afya mifumo ya utoaji huduma za afya.

Pia Dk. Mwinyi, alikipongeza Chuo kikuu cha Zanzibar kwa kuanzisha shahada ya Sayansi ya afya ya jamii na kukiahidi chuo hicho kupata ushirikiano zaidi kutoka kwa serikali ili kuhakikisha lengo la kuanzishwa fani hiyo linafanikiwa sambamba na kukitaka chuo hicho kubuni fani zenye mahitaji ya soko la ajira nchini pamoja na mipango ya maendeleo.

Aidha, aliwataka wahitimu hao kuangalia fursa zilizopo kwa nia ya kuongeza viwango vyao vya elimu. Samamba na kuwataka wageni waliopo nchini kutenga muda wa kuangalia vivutio vya Utalii vilivyomo nchini ikiwemo hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, fukwe, mashamba ya viungo, pamoja na sehemu za historia ili wakawe mabalozi wazuri wa kuisifia Zanzibar watakaporejea nchini mwao.

Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa alikitaka chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) kuongeza wigo kwenye fani za sayansi hasa kwa kada za udaktari na ufamasia ili kukuza vipaji vilivyoandaliwa tokea ngazi za maandalizi, msingi na sekondari.

Akizungumza kwenye Mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Abdul Kadir Othman Hafidh aliipongeza juhudi zinazofanywa na Rais Dk. Mwinyi katika kuharakisha maendeleo ya nchi kupitia sekta ya Elimu Zanzibar, hasa kuimarisha miundombinu ya kisasa inayotoa hamasa kwa wanafunzi kujisomea.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Juma Burhan Mohamed ambae pia ni Mkurugenzi mtendaji, Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi, aliwataka wahitimu hao kutembelea ofisi za uwezeshaji ili kujifunza kivitendo na kuangalia fursa za masoko ya ndani na nje na kujifunza jinsi ya kujitegemea.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.