Habari za Punde

Serikali Inathamini Juhudi za Taasisi za Kidini Kupeleka Huduma kwa Wananchi -- DKT. BITEKO Afariji Wagonjwa Hospitali ya San Pio Bukombe, Geita

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiangalia moja ya vifaa vya matibabu  katika Hospitali ya San Pio wilayani Bukombe mkoani Geita.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Sekta za kidini katika kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi mjini na vijijini.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 2 Januari 2024 wakati alipotembelea Hospitali ya San Pio  iliyopo wilayani Bukombe mkoani Geita akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella na viongozi wa Chama cha Mapinduzi. Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 2000 kwa
mwaka.

Kwa kutambua mchango huo wa Sekta za Kidini, Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali ipo tayari muda wote kushirikiana nao ili  kuendeleza yale wanayokusudia kuyafanya katika jamii.

Dkt. Biteko amepongeza uongozi na wafanyakazi wa Hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi, Sista Teresa Goska, kwa kutoa huduma bora za kiafya kwa wananchi   na pia uamuzi wao wa kuanza kutoa huduma katika Sekta ya Elimu ambapo wameanza na darasa la awali.

Akiwa katika Hospitali hiyo ya San Pio, Dkt. Biteko aliwafariji
wagonjwa mbalimbali waliolazwa na wanaosubiri huduma pamoja na kukagua majengo na miundombinu ya kutolea huduma hospitalini hapo.

Uongozi wa Hospitali hiyo umemshukuru Dkt. Biteko kwa kutembelea hospitali hiyo ikionesha kuwa, anatambua na kuthamini huduma inayotolewa kwenye hospitali ya San Pio ambayo ipo chini ya Jimbo
Katoliki la Kahama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.