Habari za Punde

UNICEF Yaahidi Kuwekeza Tanzania Katika Lishe kwa Watoto

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiagana na  Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, baada ya kujitambulisha ambapo walijadiliana pia maeneo mbalimbali ya kukuza ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo, Jijini Dodoma

Na. Asia Singano, WF, Dodoma.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limeahidi kuisaidia Tanzania kwenye masuala ya Lishe ili kukabiliana na Udumavu wa watoto ambao unaathari katika ukuaji wa ubongo na uchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na  Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.

Mhe. Chande, alisema kuwa Shirika hilo limekuwa likiisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya kibajeti ambapo katika mwaka wa fedha 2023/ 2024, lilitoa dola za Marekani milioni 20.3 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 50 za Tanzania.

Mhe. Chande ameliomba Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake inazozifanya kuboresha maisha ya wananchi wake na kujikwamua kiuchumi.

Aidha amelishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali na aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Shirika hilo wakati likitimiza kazi zake nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, alisema UNICEF inaahidi kuwekeza kwenye lishe ya Watoto ili kusaidia kuondoa udumavu kwa kuwa udumavu unaathari katika ukuaji wa ubongo wa mtoto na pia kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa Shirika lake linajitahidi kuhakikisha linasaidia masuala ya kibajeti na program zinazoendelea nchini Tanzania kwa kuwa lengo lao ni kusaidia katika maendeleo ya watoto na wanawake kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na UNICEF kama Wakala wake.

Bi. Wisch alisema kuwa amekuja kujitambulisha lakini pia kuelezea maeneo ambayo watawekeza kwa kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watoto pamoja na sekta za fedha.

Aidha aliipongeza Tanzania kwa ushirikiano inaouonesha kwa Shirika hilo na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo katika suala la lishe ya watoto na wanawake lakini pia suala la elimu, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akishauri kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), kusaidia masuala ya kibajeti, wakati wa mkutano kati yake na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika hilo, Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.

Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, akieleza nia ya Shirika hilo kuwekeza katika lishe kwa lengo la kuondoa udumavu na kuchochea ukuaji wa uchumi, alipokutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (hayupo pichani), kwa lengo la kujitambulisha, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akizungumza jambo wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), na  Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa nne kulia), na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka UNICEF na Tanzania, baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Naibu Waziri huyo na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.