Na Sheha Sheha. Maelezo. 26.03.2024.
Viongozi na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wametakiwa kusimamia nidhamu kazini ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza katika ziara ya kuangalia uwajibikaji na utendaji wa Taasisi hizo kwa nyakati tofauti, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka Viongozi na Watendaji kuwajibika ili kuondosha uzembe na migogoro katika sehemu za kazi.
Aidha amesema baadhi ya Viongozi wanawanyanyasa wafanyakazi wao jambo ambalo linapelekea kuwepo kwa migogoro isiokwisha na kuondosha ufanisi wa kazi.
Pia, amewataka wafanyakazi kuacha tabia ya utoro na uchelewaji na badala yake wafanye kazi kwa mujibu taratibu na sheria za kazi ili kuweza kutimiza malengo ya Serikali ya kuwataka Wafanyakazi kuwajibika.
Hata hivyo amesema Wizara haitomvumilia Kiongozi yoyote atakaebainika kutoa vitisho kwa Wafanyakazi wanaodai haki zao.
Waziri Tabia Amekiri kuwa Wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa Majengo ya Ofisi hivyo amewataka Wafanyakazi kuwa wavumilivu na Serikali ina lengo la kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto hizo.
Nao Wafanyakazi wa Wizara hiyo wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi yao kucheleweshwa stahiki zao na uduni wa miundombinu na uhaba wa wafanyakai kwa baadhi ya Taasisi hivyo wameiomba Wizara kuangalia kwa jicho la huruma.
Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amefanya ziara katika Taasisi mbalimbali za wizara hiyo ikiwemo Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu (BASSFU), Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Baraza la Vijana, Nyumba ya Sanaa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.
No comments:
Post a Comment