Habari za Punde

CDE.Mbeto -Ataka Viwanja vya Michezo Zanzibar Vitumike

Na.Mwandishi Wetu -Zanzibar.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,ameishauri Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar kuhakikisha inasimamia vizuri matumizi ya Viwanja vya vya kisasa vya michezo  vilivyojengwa na Serikali kwa ajili ya kukuza vipaji vya Vijana kupitia michezo mbalimbali nchini.

 

Ushauri huo aliutoa wakati akizindua msimu wa nne wa ligi ya mpira wa miguu ya Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe Mhe.Ameir Abdalla Ameir "Ameir CUP"  iliyozinduliwa katika Uwanja wa Magirisi Unguja.

 

Amesema Serikali imejenga viwanja vya kisasa kwa kutoa kipaumbele cha kukuza sekta ya michezo nchini.

 

Katika maelezo yake Mbeto,alisema suala la michezo limepewa nafasi kubwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ili Wananchi hasa vijana waweze kujiajiri wenyewe kupitia sekta hiyo.

 

Katibu huyo wa Kamati Maalum Mbeto,alieleza kuwa Wizara ya Habari kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) wanatakiwa kuhakikisha ligi mbalimbali zinazochezwa katika viwanja vya mitaani na zina mashabiki wengi zinachezwa katika viwanja vya kisasa ili kiibua vipaji na kuongeza kipato.

 

Alieleza kuwa Zanzibar imeendelea kutoa vijana wengi wenye vipaji vinavyokubalika katika soka la ligi za Kitaifa na nje ya Tanzania.

 

"Vijana tumieni vipaji vyetu kujiajiri mpira ni biashara na ajira sio burudani tu kwani tuangalie Kuna baadhi ya wachezaji katika ligi za Tanzania bara wanalipwa mshahara wa zaidi ya milioni 10."alisema Mbeto.

 

Alitoa wito kwa Wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kulinda miundombinu ya michezo inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa dhamira ya kunugaisha Wananchi wote.

 

Mbeto,akizungumzia suala la ligi hiyo ya "Ameir Cup'' amesema alimpongeza Mwakilishi huyo kwa kwa juhudi zake za kuanzisha ligi hiyo inayozalisha vijana wengi wenye vipaji na uwezo wa kushiriki ligi mbalimbali za Kitaifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.