Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Mwinyi Atowa Shukrani kwa Wananchi wa Bweleo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Bweleo na kutowa shukrani kwa niaba ya Familia, baada ya kumalizika kwa kisomo cha Hitma na Dua ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Mstaafu Marehemu Alhajj Ali Hassan Mwinyi, iliyofanyika leo 31-5-2024 katika Masjid Taq-wa Bweleo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuendeleza ushirikiano mwema kwa wananchi wa kijiji cha Bweleo na kufuata nyayo za Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Alhaj Dk. Mwinyi pia aliwaahidi wananchi hao kuyabeba na kuwa wajibu wake kwa yote yaliyokuwa yakitekelezwa na Marehemu Mzee Mwinyi kijijini hapo.

Al hajj Dk. Mwinyi, ametoa ahadi hizo kwenye Kijiji cha Bweleo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, mara baada ya ibada ya sala ya Ijumaa iliyofuatiwa na du’a maalum ya kumuombea Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliefariki dunia Mwezi Februari mwaka huu.

Pia, Al hajj Dk. Mwinyi aliwashukuru wanakijiji hao na Watanzania kwa ujumla kwa kuendelea muombea du’a njema mzee wao.

Akisoma risala kwenye ibada hiyo, kwa niaba ya wanakijiji cha Bweleo Maalim, Khamis Mussa ambae pia ni kiongozi wa Msikiti wa kijijini hapo, alimuomba Alhaj Rais Dk. Mwinyi na familia ya Hayati Mzee Mwinyi kwa ujumla kuendeleza ushirikiano aliouwacha Mzee wao kijijini hapo kwenye masuala mbalimbali ya jamii.

Aidha, walishikuru mambo makubwa mawili aliyofanya Mzee Ali Hassan Mwinyi  kijiji hicho na sasa yamewaletea heshima kubwa kwao ikiwemo kuwapa maeneo mawili likiwemo Jengo la vijana wa Bweleo na shaba kubwa la kinamama ambayo aliyasimamia vyema hadi aliyapatia warka nasasa wanabweleo wanayamiki kisheria.

Alisema maeneo hayo kwasasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeyaboresha kwa kujenda Chuo Cha Mafunzo ya Amali chenye tija kubwa kwa Wanabweleo na nchi kwa ujumla pia Samba la miti la Ushirika wa kina mama kwasasa Serikali inalijenga Chuo chenye hadhi na jina kubwa duniani Chuo cha IIT Madrsa ikiwa ni tawi la chuo hicho kutoka India ambacho kimeipatia Bweleo, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, heshima kubwa ndani na nje ya nchi.

Mbali na mambo mengine pia wanakijiji hao wameiomba Familia ya Marehemu Mzee Mwinyi kuendelea kuyashikilia masuala ya jamii yaliomo kijijini humo ikiwemo maulidi na dhkri za kila mwaka sambamba na kuwatembelea wazee na wanajamii hao.

Pia wanakijiji hao waliishukuru falimia ya Mzee Mwinyi kwa kuiheshimisha Bweleo siku ya Msiba wa Mzee Mwinyi kwa Mwili wake kulazwa kijijini hapo nakuthimulia mwaka 1984, alipokua Rais wa Zanzibar, Mzee Ali Hassan Mwinyi alifanya ziara ya kwanza kijijini hapo na kuweka historia na heshima kubwa ya kijiji chao kwa nyakati zote za uongozi wake akiwa mkuu wa nchi.

Mapema akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa, Khatib Sheikh, Mussa Ali Kirobo aligusia suala la Hijja na vipaombele vilivyoombwa na baadhi ya taasisi za hijja nchini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo ombi la uwepo wa usafiri wa Moja kwa moja kutoka Zanzibar hadi Makkah Saudi Arabia, kuboreshwa kwa mfumo wa hijja visiwahi ili kutoa fursa kubwa ya Mahojji wengi Kwenda kutekeleza ibada hiyo ikiwemo pendekezo la kuanzishwa kwa hesabu maalumu za benki (account) kwa kila mtoto atakayezaliwa kuanzishiwa ili akiwa na uelewe kuwepo wepesi na nafasi nyingi za watu Kwenda kuhiji akitolea mfano nchi ya Indonesia iliopo bara Asia ambao hufuata mfumo huo.

Aidha, Khatibu huyo aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa utalii wa kiislamu kwa kutoa fursa ulimwenguni kote kuja kuizuru Zanzibar kwa masuala ya dini badala ya utalii wa kawaida pekee iki kuzidi kuijengea sifa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.