Habari za Punde

MAJALIWA: SERIKALI ITAENDELEA KUIPA KIPAUMBELE SEKTA YA MICHEZO

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea tuzo ya heshima katika sekta ya michezo kutoka kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro, kwenye ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam Juni 09, 2024(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa sekta ya michezo inaendelea kuwezeshwa na kupewa kipaumbele kwa kuwa ni sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema kuwa sekta hiyo inachangia kutoa ajira kwa vijana, kuchangia pato la Taifa, inapunguza gharama za matibabu kwa maradhi yasiyoambukiza, inalitangaza Taifa Duniani, inaleta burudani na hamasa pamoja na kujenga umoja wa kitaifa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Juni 9, 2024) kwenye Hafla ya Tuzo za Michezo katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar Es Salaam, ambapo amesisitiza matumizi sahihi ya fedha zinazotengwa kwa shughuli za michezo.

“Fedha inayotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo hususan asilimia tano ya  Mfuko wa Maendeleo ya Michezo itumike kama ilivyokusudiwa ili kuendelea kuinua michezo nchini.“

Waziri Mkuu amesema katika kipindi hiki imeshuhudiwa  ongezeko kubwa la bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo kwa mwaka ujao wa 2024/2025 kutakuwa na ongezeko la kutoka shilingi bilioni 35.4 mwaka 2023/2024 hadi kufikia bilioni 285.3 sawa na ongezeko la asilimia 805.

“Hili ni ongezeko kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Wizara hii. Tumpongeze na kumshukuru sana Mhesimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini michezo na utamaduni.“

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iandae programu mbalimbali za michezo ambazo zitakuza vipaji kwa Watanzania kuanzia ngazi ya elimu ya awali.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe inashawishi uwekezaji katika viwanda vya vifaa vya michezo hapa nchini ili vifaa vya michezo vyenye ubora viweze kupatikana kwa wingi na kwa bei rafiki.

“Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zihakikishe michezo inachezwa kikamilifu katika ngazi zote za shule ikiwemo ya Awali, Msingi, Sekondari pamoja na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote wa michezo kama walivyoainishwa katika sera ya maendeleo ya michezo wahakikishe wanashiriki katika kuendeleza michezo ipasavyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema sekta ya michezo imeshuhudia mafanikio makubwa sana katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Ni kwa mara ya kwanza tunazishuhudia timu za Tanzania zikicheza kombe la dunia, kadhalika timu za vilabu hususan vya mpira wa miguu zimeweza kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika.” 

Akizungumzia kuhusu tuzo hizo, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa zina umuhimu mkubwa katika kuchagiza maendeleo ya sekta ya michezo kwa kuwapa motisha wanamichezo wanaofanya vizuri ili kuwahamasisha wengine kufanya vizuri zaidi.

“Napenda kukuhakikishia kuwa sisi kama Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa tunaendelea kuhakikisha dhana ya utawala bora ndani ya Vyama na Mashirikisho ya Michezo inasimamiwa ipasavyo.”

Amesema hadi sasa wizara yao imefanikiwa tumefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ndani ya vyama vya michezo. “Ni matumaini yetu kwa kufanikisha hilo sekta ya michezo itapata msukumo mkubwa zaidi wa maendeleo.”

Katika hafla hiyo Baraza la Michezo Tanzania (BMT) lilimpatia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tuzo ya utambuzi ya mchango wake katika sekta ya michezo. Tuzo hiyo alikabidhiwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, JUNI 10, 2024.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.