Habari za Punde

muhimu kwa jamii kushikamana na tabia za watu wema

Mkoa wa Mjini Mgharib Na. Mwandishi OMKR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa jamii kushikamana na tabia za watu wema kwa kuwa ni maagizo kutoka kwa Mwenyezimungu muumba, katika kufikia kupatikana daraja kubwa za kheri kwa duania na akhera.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko Kiponda mjini Zanzibar alipotoa salaam kwa waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria katika khitima ya kumuombea dua marehemu Mohammed Raza ambaye jana ametimiza mwaka mmoja tokea alipofariki dunia.

Amesema watu wema bila kujali kipato walichonacho ama darja yao katika jamii au nyadhifa za siasa wanajishusha kwa nia ya kujiweka pamoja na jamii sambamba na kuwasaidia wenzao kwa kila walichoruzukiwa na mwenyezimungu kwa kuwa ndio njia mojawapo muhimu ya kutekeleza ibada.

Alisema tabia za Marehemu Raza zilijeweka katika akhalaki njema kwa kuishi na watu kwa amani na kwasaidia wengi bila kujali ikiwa ni pamoja na kuishi nao kwa kuchanganyika na jamii zote katika mazingira tofauti licha kwamba mungu alimruzuku wasaa  mkuwa  wa kipato kuliko walivyowengi.

Amesema kwamba iwapo jamii itashikamana na kuishi katika hali kama hiyo ya kushikamana na tabia njema ya kumjali kila mmoja ni elimu na darsa kubwa kwa waumini na ni hatua ya kujijengea khatima njema katika kupata malipo mema ya akhera kutoka kwa mola muuumba.

Mhe. Makamu amesema kwamba watu wenye tabia njema wametukuzwa na mwenyezimungu ikiwa ni pamoja na kuwa na watoto wenye kuwaombea dua wazazi wao  waliotangulia mbele ya haki ili kuendeleza mema yao waliyoyaacha na ujira wao kutoka kwa mungu uweze kuendelea.

Amefahamisha kwamba hali hiyo sio tu kwamba huleta furaha kwa wanajami lakini pia husaidia nchi kuwa na Amani na kuwepo mshaikamano wa umma katika kuleta maendeleo ya taifa lao na kwamba Raza alijitaihdi kuwa pamoja na watu.

Amesema kwamba marehemu Raza pamoja na kuwa na mali nyingi, lakini aliishi katika maisha ya maagizo ya vitabu vitakatifu kwa kutokushughulishwa sana na mali hiyo  na badala yake alifanya mengi ya kusaidia kama ujenzi wa misikiti , madrasa na vituo vya afya jambo lililomfanya kuweka alama njema katika kupeleka mbele dini kwenye maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Naye Mhadhiri wa kimatiafa katika mihadhara ya Kiislamu kutoka Landon Sayyed Ammar amesema kwamba  alichofanya Marehemu Raza ni kuweka Uzanzibari wake mbele kwa kuipenda nchi yake na kufanya hivyo ni kutekeleza ibada kupitia nguzo ya imani jambo ambalo linahitaji kufanywa na waumini wote.

Akitoa shukran kwa niaba ya waliohudhuria kwenye dua hiyo Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mambo ya siasa Mhe. Haji Omar Kheir, alishauri wanafamilia kushirikiana na wataalamu mbali mbali kuyaandikia kitabu mema yote aliyoyafanya marehemu Raza.

Naye Mtoto Mkubwa wa Marehemu Hassan Raza, akitoa shukrani kwa niaba ya familia amewashururu viongozi  , wananchi na watu mbali mbali kwa kuwa pamoja katika kumuombea dua marehemu baba yao na kueleza kwamba katika kuendeleza mambo mema aliyokuwa akiyafanya baba yao wapo kwenye hatua za mwisho kusajili fondesheni ya kuweka kielelezo cha kumuenzi  mzee wao huyo.

Mwisho.

Kitengo cha Habari.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Juni, 09.06.04.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.