Na Khadija Khamis- Maelezo . 20/07/2024.
Waziri wa Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka Wakandarasi wa mradi wa Ujenzi wa Jengo la Shirika la Magazeti (Zanzibar leo) kusimamia matakwa yaliyomo kwenye mkataba ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Ameyasema hayo huko Tunguu Wilaya ya Kati Unguja wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo na hatua zilizofikia za ujenzi huo.
Amesema mradi huo umeshafikia asilimia 30 hadi sasa na kuishajihisha Kampuni ya ujenzi huo Skyward Construction kumaliza kabda ya muda ulioweka kutokana na hatua, spidi pamoja na uwezo wa Kampuni hiyo .
“Nakushajihisheni kuwa pamoja na kwamba mkataba umesema ujenzi utamalizika mwezi wa tisa 2025,nakuombeni mufanye kazi kwa spidi tumalize kabla ya muda huo .”amesema Waziri Tabia .
Waziri Tabia alimtaka Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti Ali Haji Mwadini kuwa karibu na Wakandarasi ili kuweza kutatua changamoto kwa haraka pindipo zikijitokeza .
Akitoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo amewaomba kutoa mashirikiano kwa wakandarasi ili kufanikisha mradi huo kwa wakati uliopangwa .
Nae Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti Zanzibar Ali Haji Mwadini amesema utapokamilika ujenzi huo utaleta ufanisi mkubwa katika Shirika hilo jambo ambalo litatoa fursa ya kutumia mitambo yake wenyewe ya kutengenezea magazeti .
Sambamba na hayo jumla ya familia nane za watumishi wa shirika hilo watapatiwa nyumba za kuishi katika eneo hilo jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi .
Amefafanua kuwa mradi huo utajumuisha Jengo la Ghorofa nne, Nyumba za Watumishi zitakuwa na ghorofa moja, ambazo zitachukuwa familia nane, Kiwanda cha Magazeti , pamoja na Msikiti
Kwa upande wa Mshauri elekezi wa Wakala wa Majengo Abubakar Mohamed Bakari ameahidi kusimamia ujenzi huo na kuhakikisha unamaliza kwa muda muafaka na kiwango kilichokusudiwa .
Jumla ya Shilingi Billion 8.1, 2 zitatumika kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umeanza kutekelezwa mnamo Mwezi Machi mwaka 2024 na kutarajiwa kumalizika Septemba 2025.
No comments:
Post a Comment