Habari za Punde

Makalla: CCM inahitaji subira


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla akizungumza na Wanachama pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni katika Ukumbi wa Kiramuu Hall, leo NOV 04, 2024. (Picha na Fahadi Siraji)

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla ametoa wito kwa waliyokuwa wagombea wa chama hicho katika nafasi za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao majina yao hayakupitishwa pamoja na kwamba walishinda kura za maoni, kuwa na Subira..

Makalla ameyazungumza hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa chama hicho Wilaya ya Kinondoni.

Pia amewapongeza baadhi ya wagombea ambao majina yao yalikatwa na bado wanaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama hicho, akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuna kipindi aligombea na kushinda kwa kishindo lakini jina lake halikurudi.

“Tunawatakia kila la kheri waliokosa uvumilivu, wako ambao hata uteuzi haujafanyika wakahamia mtaa wa pili siku ya tatu wakageuza tena CCM, niwape salamu hao waliowaokoteza tumewaazima tuu wagombea watarudi Chama cha Mapinduzi,” alisema na kuongeza:

“Kuna wengine hata vikao hatujakaa niliona wanakaribishwa siku mbili jamaa akarudisha kadi akarudi CCM, hivyo niwaombe kuweni watulivu tuna uchaguzi mwakani,” amesema Makalla.

Aidha, amesema uchaguzi wa awamu hii hauna kupita bila kupingwa, hivyo waombea na wanachama wa chama hicho wasibweteke, akisisitiza kwamba wako imara na hawatalala.

Amesisitiza kwamba watahakikisha hata pale watakapokuwa wako pekeyao watafanya kampeni na kuhakikisha wagombea wao wanapata kura za ndio.

“Anaesubiri kumuangusha mgombea wa CCM kwa kura za hapana ni sawa na mtu anaesubiri ndege bandarini badala ya ‘Airport’ wanaccm nchini kote tuchangamke hakuna neno ‘Mama’ tukamilishe hiyo kazi, mahali patakapothibitika tuko sisi tutafanya kampeni ya kutosha wagombea wetu wote wapite kwa kishindo,” amesema Makalla.

Mwisho

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.