Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akishiriki katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliyofanyika pembezoni mwa
Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini
Marekani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inasisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa kukabiliana na dharura za afya ya umma barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliyofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Amesema Tanzania imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuimarisha masuluhisho ya kibunifu ya ufadhili pamoja na kuunga mkono mipango ya kikanda ambayo inapunguza utegemezi wa misaada kutoka nje, na hivyo kuhakikisha kuwa vipaumbele vya afya vya Afrika vinashughulikiwa na serikali za Afrika.
Aidha, Makamu wa Rais amesema uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu, na bidhaa nyingine muhimu za matibabu ni muhimu katika kujitegemea kweye sekta ya afya. Amesema Tanzania inahimiza uwekezaji katika viwanda vya ndani, mamlaka ya udhibiti ya pamoja barani kote, na ubia wa uhawilishaji wa teknolojia ili kuimarisha uwezo wa Afrika wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.
Amesema kufuatia uzoefu wa hivi karibuni wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ikijumuisha Marburg na vimelea vingine vinavyoambukiza, yametoa hitaji la kujiandaa kwa nguvu na mifumo ya kukabiliana na maradhi.
Ameongeza kwamba Tanzania inasaidia vitengo vya matibabu ya magonjwa ya kuambukiza, upelekaji wa haraka wa timu za dharura, na uwekezaji katika miundombinu ya wafanyikazi na afya.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, udhibiti wa maambukizi, vifaa, na uratibu kwa ajili ya kukabiliana na milipuko kwa wakati na kwa ufanisi.
Pia, Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Jumuiya za kiuchumi za kikanda, na Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Afrika ili kuwa na mbinu ya pamoja ya kukabiliana dharura za afya.
Amesema ushirikiano katika uchunguzi, sera na mipango ya pamoja ya kujenga uwezo itaimarisha uwezo wa pamoja wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na vitisho vya afya vinavyojitokeza.
Mkutano
wa Kamati hiyo umelenga kujadili masuala yanayohusu Kituo cha
Kudhibiti Maradhi Afrika (Africa CDC), chini ya kauli mbiu isemayo ‘Kuhakikisha
Uhuru wa Afya Afrika: Uongozi wa Kisiasa kwa Ufadhili Endelevu wa Sekta ya
Afya, Uzalishaji wa Ndani na Maandalizi dhidi ya Milipuko ya Maradhi.
Imetolewa na
Ofisi ya
Makamu wa Rais
23 Septemba
2025
New York –
Marekani.
No comments:
Post a Comment