Habari za Punde

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipofungua Maonesho ya Teknolojia ya Madini Kwenye viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mjini Geita, Septemba 22, 2025. (PIcha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU,Kassim Majaliwa amesema kuwa Sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo ya uchumi nchini ambapo katika mwaka 2022 sekta hiyo imekua kwa asilimia 10.9 na kufikia mchango wa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 9.0 mwaka 2023.

 

Ametoa kauli hiyo Leo (Jumatatu, Septemba 22, 2025) wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini Mkoa wa Geita, yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Amesema kuwa hatua hiyo imetokana na jitihada mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita ikiwemo kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara ya madini,  matumizi ya mifumo ya kielektroniki (online mining cadastre system), uwepo wa masoko ya madini na ufuatiliaji wa mikataba ya uwekezaji.

 

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya madini ili rasilimali za madini zichangie kwa katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa Watanzania wote".

 

Waziri Mkuu ametoa rai kwa wadau wa sekta ya madini kuendelea kuwekeza katika teknolojia kwani ndiyo daraja la mageuzi kuanzia utafiti na uchimbaji, usafishaji na biashara ya madini. "Bila teknolojia sahihi, haiwezekani kuongeza tija, kuhakikisha usalama wa wachimbaji, kulinda mazingira, wala kufanya uongezaji thamani wa madini yetu".

 

Ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, katika kiipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 Wachimbaji wadogo wa Geita wamezalisha zaidi ya kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.44, huku Serikali ikipata zaidi ya Shilingi Bilioni 235.5 kama mrabaha. "

 

Aidha, makampuni makubwa kama Geita Gold Mine na Buckreef katika kipindi hicho wamezalisha kilo 76,530 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Trilioni 11.38, na Serikali kupata zaidi ya Shilingi Bilioni 793 kama mrabaha."

 

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tanzania sasa imepiga hatua kwa kuwa na viwanda vya kutengeneza zana mbalimbali za uchimbaji wa madini.

 

"Katika mwaka wa fedha 2024-2025 tumeweza kuzalisha tani 62 za dhahabu tofauti na nyuma tulikuwa tukizalisha tani 40-50 kila mwaka hii inatufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano bora Afrika katika uzalishaji wa dhahabu."

 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema huo umefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini na kwa kuwa kazi ya uchimbaji unahitaji umeme tayari umeme umepelekwa katika maeneo mengi ya wachimbaji wadogo.

 

"Tumefanyia kazi maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo ili wafanye kazi zao na kuwa na uzalishaji wa uhakika katika maeneo yao."

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

JUMATATU, SEPTEMBA 22, 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.