WAJUMBE wa kamati tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), leo wanatarajiwa kupiga kura kumchagua Rais mpya atakayekiongoza chama hicho kwa kipindi kilichobakia hadi wakati wa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka 2014.
Uchaguzi huo mdogo unafanyika kufuatia hatua ya Rais wa zamani Ali Ferej Tamim, kujiuzulu wadhifa huo tangu Machi 2, mwaka huu, ambapo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, anatarajiwa kuufungua.
Hata hivyo, uchaguzi huo unafanyika huku kukiwa na mgombea mmoja pekee, Amani Ibrahim Makungu, baada ya Salum Bausi Nassor ambaye pia alichukua fomu kwa ajili ya kuwania kiti hicho, kujiondoa kwa madai ya viongozi wa ZFA kukiuka maadili.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa ZFA Munir Zakaria, uchaguzi huo umepangwa kufanyika wakati wa saa 7:00 mchana katika ukumbi wa 'Roof top' hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.
Tayari wajumbe wa kamati hiyo kutoka Pemba, wamewasili mjini hapa tangu jana mchana kukamilisha idadi ya wajumbe 55, wanaotarajiwa kutumia haki ya kupiga kura ili kujaza nafasi hiyo iliyobaki wazi kwa miezi mitatu sasa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Katibu wa kamati ya uchaguzi Afan Othman Juma, amesema kila kitu kiko sawa na kinachosubiriwa ni muda ufike ili kutekeleza azma ya kumtafuta Rais mpya wa ZFA.
Jana asubuhi, mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa Dar es Salaam, aliwashuhudia baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji ya ZFA walioko na timu zao zinazoshiriki michuano ya Copa Coca Cola akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho Wilaya ya Mjini Yahya Juma Ali, wakiziacha timu hizo na kupanda boti ya Kilimanjaro III, kurudi Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura.
0 Comments