6/recent/ticker-posts

Ratiba 'Kagame Cup' hadharani. Yanga kuanza na Atletico ya Burundi L Mafunzo, Azam FC kundi moja








Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
YANGA, inayokabiliwa na kibarua cha kutetea ubingwa wa klabu Afrika Mashariki na Kati kupitia mashindano ya  Kombe la Kagame, itaanza kampeni zake Julai 14 mwaka huu kwa kuwavaa wawakilishi wa Burundi, timu ya  Atletico kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Timu 11 zinatarajiwa kushiriki patashika hizo, zitakazoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu, huku kila siku zikichezwa   mechi mbili, saa 8 mchana na saa 10 jioni, ambapo mbali na Yanga, Tanzania Bara itawakilishwa pia na klabu za Simba na Azam.
Ratiba ya mashindano hayo inaonesha kuwa, mechi ya kwanza siku ya ufunguzi ambayo itachezwa saa 8:00 mchana, itazikutanisha timu za APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini.
Katika kundi A la michuano hiyo, kutakuwa na timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti, ambapo Azam FC, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko katika kundi B.
Kundi C linaundwa na timu za Yanga, APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi.
El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali.
Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kati ya Julai 13 na 15.
Fedha za zawadi kwa bingwa wa michuano hiyo hutolewa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambapo bingwa atazoa  dola elfu 30, makamu bingwa dola elfu 20 na mshindi wa tatu dola elfu kumi.
Michuano hiyo itaoneshwa moja kwa moja na televisheni ya Super Sport.

Post a Comment

0 Comments