Na Ameir Khalid
MASHINDANO ya Kombe la Urafiki Tanzania, yanayotarajiwa kuanza kesho kwenye uwanja wa Amaan, yameingia dosari baada ya klabu ya Yanga kutangaza kujiondoa.
Msemaji wa klabu hiyo Louis Sendeu ameliambia Zanzibar Leo kwa njia ya simu jana, kuwa watakuwa tayari kushiriki michuano hiyo, kama waandaaji wake watakubali kuyasogeza mbele hadi baada ya mashindano ya Kagame yanayotarajiwa kuanza mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Amefahamisha kuwa, kwa sasa timu yake inatoa umuhimu mkubwa kwa michuano ya Kagame ambayo Yanga ni bingwa mtetezi, na kuongeza kuwa wanathamini hadhi ya Kombe la Kagame, ambalo wanalazimika kulitetea kwa nguvu zote.
Alieleza kuwa tayari masharti hayo wameshayaeleza kwa ZFA lakini hadi sasa chama hicho kimekaa kimya na hakuna dalili yoyote ya kukubali ombi hilo.
Alipoulizwa, Ofisa Habari wa ZFA Miunir Zakaria, alikiri kuwa Yanga imejiondoa kwenye michuano hiyo, lakini akasema ZFA ndiyo yenye mashindano na hakuna klabu inayoweza kuipangia namna ya kuyaendesha.
Hata hivyo, hakuwa tayari kueleza mara moja kama wataalika timu mbadala, huku Katibu wa kamati ya mashindano Suleiman Mahomud Jabir, akimtaka mwandishi wa habari hizi kutomuuliza lolote juu ya michuano hiyo, kwa vile anauguliwa na nduguye, na kwamba alikuwa kwenye harakati za kushughulikia matibabu yake.
Wakati Yanga ikijitoa, Simba na Azam zimethibitisha kushiriki kwenye michuano hiyo, huku Simba ikitarajiwa kuwasili leo hapa Zanzibar tayari kwa ngarambe hizo.,
Msemaji wa Simba Ezekiel Kamwaga, amesema kushiriki kwao katika michuano hiyo, si kwa lengo la kutaka kuchukua ubingwa ingawa hilo likitokea watafurahi, bali ni kwa ajili ya kuwapa mazoezi wanandinga wa timu hiyo inayojiandaa na mashindano ya Kagame yanayotarajiwa kuanza jijini Dar es Salaam katikati ya mwezi ujao.
Wekundu hao wa Msimbazi walioko kwenye kundi A pamoja na timu za Mafunzo, Azam FC na Zanzibar U-23, watatupa karata yao ya kwanza katika michuano hiyo Julai 2, kwenye uwanja wa Amaan kwa kukwaruzana na walinzi wa wafungwa, Mafunzo mnamo saa 10. 00 za jioni.
Naye Nassor Idrisa 'Father', ambaye ni Katibu Mkuu wa Azam, alikuwa na kauli sawa na ya Kamwaga, ingawa alisema kimsingi Azam inalenga kutwaa taji ili kuweka rikodi ya kubeba vikombe viwili ambavyo mashindano yake yanaandaliwa Zanzibar, kikiwemo cha Mapinduzi ilichokibeba mwezi Januari mwaka huu.
Michuano hiyo inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ikidhaminiwa na hoteli ya Zanzibar Ocean View na duka la samani la Royal Furniture, imepangwa kuanza kutimua vumbi kesho, kwa mchezo utakaozikutanisha timu za Yanga na Jamhuri mnamo ya saa 10:00 jioni.
0 Comments