6/recent/ticker-posts

CCM Yasikitishwa na Wanaomchafua Balozi Seif.

Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesikitishwa na kulaani kauli za udhalilishaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa nchini dhidi ya Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambae pia ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba, kauli hizo za kumsakama hutolewa mara kwa mara kupitia majukwaa ya kisiasa, semina na makongamano.
Alisema lengo sio tu kumvunja moyo bali pia ni kumvunjia heshima mbele ya jamii nzima.

Alisema CCM kinachukua nafasi hiyo kumpongeza kwa dhati kwa kutekeleza vyema majukumu makubwa aliyopewa na taifa katika kusimamia shughuli zote za serikali na kwamba chama hicho kipo tayari kumpa kila aina ya msaada.

Alisema Balozi ni kiongozi mchapa kazi, asiependa mapumziko wala kujali muda na anaependa kuchanganyika na watu wa rika na jinsia zote.
Aidha alisema ni kiongozi anaejali, kusikiliza na kutatua shida mbali mbali zinazowagusa wananchi.

Alisema akiwa Mtendaji Mkuu wa serikali ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, amekuwa mstari wa mbele kutatua kero za kijamii ikiwemo migogoro ya ardhi na kuipatia ufumbuzi wa kina.

Alisema ameweza kusimamia masuala ya elimu, afya umeme, maji na miundombinu ambapo kwa kiasi kikubwa sekta hizo za nyengine zimeboreka na kuleta manufaa makubwa kwa Zanzibar.

Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, alisema CCM kinawataka wanasiasa hasa wa kambi ya upinzani kufahamu kuwa mchakato huo utakamilika kwa mujibu wa sheria na kwamba kitendo cha Wabunge wa upinzani kutoka ndani ya bunge kamwe hakitozuia mchakato huo kuendelea.

Post a Comment

1 Comments

  1. Haya ndiyo matatizo yetu CCM, kuchagua viongozi wa chama kwa kuangalia historia ya wazazi wao! na sio umahiri wa mtu kulingana na wakati uliopo!

    Kiasi fulani nakubaliana na Bi Waride kwamba lawama dhidi ya Balozi Seif Ali Iddi si sahihi lakini ni juu ya Balozi mwenyewe kujibu tuhuma hizo tena kwa hoja makini..

    Mimi bado naamini kama atafanya hivyo basi watu watamuelewa tu! hata kama sio wapinzani basi sisi tutamuelewa!

    Ubaya wa kumtumia katibu wenezi kujenga hoja nyepesi nyepesi, kunaweza kuwafanya baadhi ya wananchi kuamini kwamba tuhuma dhidi ya Balozi ni za kweli, kitu ambacho ni uzushi!

    ReplyDelete