6/recent/ticker-posts

Dk Shein atuma salamu za rambi rambi kwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Jamhuri ya Watu wa Kenya Bwana Uhuru Kenyatta kufuatia shambulio la kigaidi lililotokea kwenye eneo la maduka la Westgate lililopelekea vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.
Katika salamu zake hizo, rais wa Zanzibar amesema yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa mshtuko mkubwa na wamehuzunishwa na tukio hilo la kigaidi na kikatili kwenye eneo la maduka la Westgate mjini Nairobi.
Amesema wananchi wa Zanzibar wanaungana na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na ndugu zao wa Kenya katika kuomboleza vifo vya maafisa wa usalama na wananchi wa Kenya na wote waliopoteza maisha yao kutokana na tukio hilo. Aidha, alisema wananchi wa Zanzibar wanaungana na wananchi wa Kenya na watu wote kulaani vitendo hivyo vya kigaidi.
Katika salamu hizo, Rais wa Zanzibar amewaomba wananchi wa Kenya kuwa na subra na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, amewatakia malazi mema peponi waliofariki kutokana na janga hilo,  na amewaombea kupona haraka wale waliojeruhiwa kutokana na tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments