Na Said Ameir, Ikulu
Mkurugenzi wa IFAD wa Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika Bwana Perin Saint ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutekeleza vyema programu ya Huduma za Kilimo na Maendeleo ya sekta ya Mifugo (ASSP/ASDP–L)
nchini.
Mkurugenzi huyo ambaye alifika Ikulu kusalimiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza azma ya IFAD YA kufanya mkutano wake mkuu wa mwaka huu hapa Zanzibar kutokana na Mfuko huo kuridhika na mazingira yaliyopo nchini.
Amesema Zanzibar imekuwa nchi ya mfano katika kutekeleza programu za Huduma za Kilimo na Maendeleo ya sekta ya Mifugo (ASSP/ASDP–L) zinazogharamiwa na mfuko huo katika Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, na kwamba IFAD imeridhishwa na hatua ya serikali katika kusimamia programu hizo.
Amesema kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa program hizo, Shirika lake linatarajia kuongeza muda wa miradi hiyo hapa Zanzibar. Programu hizo ambazo zimegharimu kiasi ya dola milioni tisa za Marekani (USD milioni 9), zilianza kutekelezwa mwaka 2007 na zinatarajiwa kumalizika mwaka 2014.
Bwana Perin L. Saint Ange amesema ameshuhudia maendeleo makubwa katika sekta mbali mbali siyo tu katika kilimo, lakini vile vile katika sekta za utalii, mazao ya viungo na mazao ya baharini, jambo ambalo amesema ni ishara ya mafanikio makubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar.
1
Aidha, amesema ameona mafanikio yaliyopatikana katika mazao mbali mbali lakini hasa zao la vanila ambalo alisema litasaidia katika kuongeza idadi ya viungo na hivyo kuifanya Zanzibar kuongeza umaarufu wake katika mazao ya viungo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa huu ni wakati muafaka kwa Zanzibar kuelekeza nguvu zake katika mazao ya baharini kwani alisema, nchi za visiwa zina fursa ya kipekee katika kuendeleza uchumi huo, na kwamba Mfuko wa Kimataifa Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika imeweka kipaumbele kwenye uchumi wa aina hiyo.
Ameongeza kuwa jumuiya za kimataifa zimeonesha hamu kubwa ya kuendeleza na kusaidia nchi za visiwa katika kuwekeza kwenye uchumi wa baharini hivyo ameitaka Zanzibar kuichangamkia fursa hiyo.
Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema mafanikio makubwa yanayoonekana katika kuimarisha kilimo na mazao ya baharini yanatokana na utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Akizungumza na ujumbe huo, Dk. Shein amesema serikali imejipanga vizuri katika kuleta Mapinduzi ya kilimo na Mapinduzi ya uvuvi ambapo mkazo zaidi
umewekwa katika kuimarisha ukulima wa mwani, ufugaji wa samaki na uvuvi wa bahari kuu.
Amesema uimarishaji wa sekta ya uvuvi ulianza zamani kwenye miaka ya sabiini,
lakini ulionekana kupungua kasi kwa kipindi kirefu kutokana na changamoto mbali
mbali kabla ya serikali anayoiongoza kuamua kuishughulikia kikamilifu sekta ya
kilimo na uvuvi.
“Serikali ilidhamiria kuiendeleza sekta ya uvuvi tokea kwenye miaka ya 70, lakini
kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo fedha, tulishindwa kufanya vizuri
kwa muda mrefu, na sasa tumeanza kupata matumaini katika utekelezaji wa
mpango wa serikali wa miaka mitano” alisema Dk. Shein.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa kuna samaki wengi katika bahari ya Zanzibar
kama vile Jodari ambao wanahitajika sana kwenye soko la dunia, lakini wavuvi
2
wa Zanzibar wanashindwa kuwavua samaki hao kutokana na kushindwa kuvua
kwenye maji ya kina kikubwa na kutokuwa na vifaa vinavyohitajika kuvua samaki
hao.
Aliufahamisha ujumbe huo kwamba serikali tayari imeshachukua juhudi mbali
mbali za kuimarisha sekta ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kutiliana saini makubaliano
ya kuiendeleza sekta hiyo na nchi ya China na Vietnam.
Kuhusu zao la mwani, Rais wa Zanzibar amesema maendeleo makubwa yameanza
kupatikana katika zao hilo kutokana kuweza kuongezewa thamani, ambapo
mwani umekuwa malighafi ya kutengenezea supu, keki na vitu vingine mbali
mbali.
Katika ujumbe wake Bwana Perin Saint Ange alifuatana na Mkurugenzi wa
Divisheni ya Ufundi anayefanyia kazi zake nchini Italia Bwana Adolf Bizzi, Mratibu
Mkuu wa Masuala ya Uchumi wa Kanda Bwana Godfrey Livingstone, Mratibu
mkuu wa Mradi nchini Tanzania Bwana Francisco Pichonkuu, Meneja wa Mradi
nchini Tanzania Bibi Mariam Okongo na Afisa wa mradi huo nchini Tanzania Dr.
Mwatima Abdalla Juma.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 E-mail:
saidameir@ikuluzanzibar.go.tz & sjka1960@hotmail.com
0 Comments