Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Rafii Haji Makame (kulia) akitoa ufafanuzi wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa UNICEF yaliyofanyika Ofisi ya Tume ya Utangazaji Kikwajuni
Ujumbe wa UNICEF ulipokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo katika Ofisi ya Tume ya Utangazaji Kikwajuni jana.
(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Khadija Khamis na Patima Mtumwa – Maelezo Zanzibar 25/09/2013.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto UNICEF limeonyesha azma ya kuendelea kusaidia kutoa taaluma katika nyanja za Afya, Elimu na Jamii nchini.
Shirika hilo kupitia Taasisi za Habari na Mawasiliano limeahidi kusaidia katika kuaandaa vipindi vya Radio na TV kwa lengo la kuelimisha jamii mjini na vijijini.
Maafisa wa Shirika hilo wakiongozwa na Mkurugenzi wake Elephase Kamugushi wameeleza hayo walipokutana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Rafii Haji katika ukumbi wa Tume ya Utangazaji Kikwajuni mjini Zanzibar .
Kamugisha ametaka vipindi hivyo vielekezwe katika kuelimisha matatizo yanayowakabili watoto ikiwemo ajira za watoto, watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na maradhi yanayowasumbua watoto ikiwemo cholera, malaria na utapia mlo.
Amesema UNICEF litasaidia upatikanaji wa nyenzo za kufanyia kazi na utaalamu ili kuviwezesha vipindi hivyo kuwa na mvuto kwa wasikilizaji.
Kamugisha ameahidi kukutana na Wizara na Taasisi zinazoshughulikia watoto Zanzibar ili kuhakikisha azma hiyo ya UNICEF inafanikiwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Rafii Haji Makame alieleza kufarijika na uamuzi huo wa UNICEF ambao umeleta faraja hasa wakati huu ambapo Zanzibar inaandaa vipindi mbali mbali kwa ajili ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi.
Alisema Idara ya Habari Maelezo imeanzisha utaratibu wa kuonyesha vipindi vijijini kwa njia ya senema na kumekuwa na upungufu mkubwa wa vipindi, hivyo msaada wa UNICEF utasaidia kupatikana kwa vipindi vya uhakika.
Mkurugenzi Rafii amelishukuru Shirika hilo kwa msaada wake huo na ameahidi kusimamia kikamilifu kuhakikisha vipindi vinavyowahusu watoto vinaandaliwa kwa wingi.
0 Comments