6/recent/ticker-posts

Wakaazi wa Paje walalamikia baa na kumbi za starehe

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk akizungumza na wananchi na wamiliki wa kumbi za starehe wa kijiji cha Paje Wizarani kwake Kikwajuni jana.
 Wananchi wa Kijiji cha Paje wakimsikiliza Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na michezo Saidi Ali Mbaouk walipokuwa na mazungumzo ofisini kwake Kikwajuni jana.
Wamiliki wa kumbi za starehe katika kijiji cha Paje wakimsikiliza Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo walipokuwa na mazungumzo ofisini kwake Kikwajuni jana.
(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).

Khadija Khamis na Patima Mtumwa – Maelezo Zanzibar. 25/09/2013.
 
Wananchi wa Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja wamewalalamikia wamiliki wa baa na kumbi za starehe zilizomo katika kijiji hicho  kutokana  na vitendo viovu vinavyo kwenda kinyume na  heshima na maadili ya kijiji hicho. 
 
Wananchi hao wametoa malalamiko yao katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk na wamiliki wa baa zilizomo kijiji hapo uliofanyika Ofisini kwa Waziri Kikwajuni.
 
Walisema wamiliki wa baa na kumbi za starehe wamekua wakiwasumbua  kwa kupiga disco usiku kucha na kusababisha kushindwa kulala majumbani mwao.


Waliongeza kuwa  tabia hiyo inapelekea vishawishi kwa watoto wao  na kujiingiza katika   mambo maovu  yanayokwenda kinyume na mila silka na utamaduni wa kijiji chao.
 
“Disco linatuletea usumbufu mkubwa kwa watoto wa kijiji chetu wapo baadhi  hawalali makwao usiku mzima,” alisema Mbaraka Salum askari Jamii wa kijiji hicho.
 
Mbaraka alisesema  vitendo vya ngono  na kubakwa kwa watoto wa kiume vimekuwa vikifanywa bila woga  na vijana 30 wa kijiji hicho tayari wameshaambukizwa virusi vya ukimwi.
 
 Wananchi hao wa Paje wameishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuzuia vibali vya kupiga Disco kumbi zote za starehe ndani ya kijiji hicho kwa kuhofia kutokea madhara makubwa zaidi.
 
Wamiliki wa Baa na kumbi za starehe kwa upande wao  wameitaka serikali iwaangalie kwa jicho la huruma kwa sababu burudani  ya ngoma ndiyo inayopelekea  kupata wateja na  kuongeza kipato chao kinyume chake ni hasara katika biashara yao.
 
‘’Tunaiomba Serikali  ituruhusu  japo siku moja kwa wiki tupige ngoma ili  tuweze kuingiza  mapato,”alisema  Mariyam Simba Mkwasi mmiliki wa baa la Vuvuzela.
 
Waziri  wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe, Said Ali Mbarouk  alisema kuwa vibali vya  musiki  vitaendelea kuzuiliwa ikiwa  wamiliki wa sehemu hizo  watashidwa kufuata taratibu ziliziowekwa .
 
‘’Ni bora tukose mapato  Serikalini  kuliko kuendelea kuwanyima uhuru wananchi wetu tutaendelea  kuzuiya vibali vya disco mpaka mujenge kumbi zisizotoa sauti,‘’alisema Waziri wa Habari.
 
Alisema iwapo kuimarika kwa sekta ya  utalii  Zanzibar kutasababisha Utamaduni wake  kumongonyoka hilo halitawezekana na hatuwezi kupanda mbegu ya ufuska katika visiwa vyetu.
 
Alisema  Zanzibar ina ustaarabu  na utamaduni wake, hivyo ametaka kila mmoja ahakikishe kuwa utamaduni huo unalindwa, unadumishwa na  kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
 
Kumbi za starehe na burudani zilizolalamikiwa zaidi na wananchi wa kijiji cha Paje ni pamoja na Vuvuzela, Jambo, Gereje na Deman Loge


Post a Comment

0 Comments