Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na Chuo Kikuu cha Haukeland katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Akizungumza na Profesa Stenner Kvisland kutoka hospiltali ya Chuo Kikuu cha Haukeland, Norway ofisini kwake Ikulu jana Dk. Shein amesema mchango wa chuo hicho kwa hospitali ya Mnazi Mmoja unasaidia utekelezaji wa lengo la Serikali kuibadili hospitali hiyo kuwa ya rufaa.
Chuo Kikuu cha Haukeland na hospitali ya Mnazi Mmoja mwaka 2009 zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano ambapo chini ya makubaliano hayo Chuo Kikuu hicho kitasaidia Hospitali ya Mnazi Mmoja kujenga uwezo katika rasilimali watu na miundombinu.
Dk Shein ameueleza ushirikiano huo kuwa ni kielelezo thabiti cha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Norway.
“Ushirikiano kati ya taasisi zetu hizi mbili ni kielelezo cha uhusiano uliopo kati ya nchi zetu mbili na kwamba msaada wenu ni hatua muhimu kusaidia kutekeleza shabaha ya Serikali yetu ya kuibadili hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa iliyokamilika” Dk. Shein alieleza.
Alieleza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo sio tu kuwa utaongeza kasi ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuimarisha hospitali ya Mnazi Mmoja bali pia utasaidia utaimarisha utoaji huduma katika sekta nzima ya afya.
Rais alieleza kuwa amefarijika kuona kuwa ushirikiano wa taasisi hizo tayari umeonyesha ishara nzuri za mafanikio ambapo jitihada zimeanza kwa kuimarisha vitengo vya magonjwa ya akili pamoja na magonjwa ya figo.
“lengo letu ni kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wanapatiwa huduma katika hospitali zetu humu nchini ili kuepukana na gharama na usumbufu wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alimueleza Profesa Stener kuwa wananchi wana matumaini makubwa na mipango ya Serikali ya kuimarisha sekta ya afya hivyo Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha malengo ya afya yanafikiwa kwa kushirikiana na washirika mbalimbali.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Norway kwa misaada yake ambayo imekuwa ikiipatia Zanzibar katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu nishati, maji na mafunzo.
Dk. Shein alikipongeza Chuo Kikuu cha Haukeland kwa kutoa fursa za masomo na mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa wataalamu wa afya wa Zanzibar hatua ambayo amesema itasaidia pia katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuanzisha Kitivo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
“Tayari tumeanzisha kitivo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Taifa za Zanzibar na masomo yanatarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwak huu. Kwa kuanzia tutadahili wanafunzi wapatao 40 hivyo mpango wenu wa mafunzo ya ngazi ya shahada ya pili kwa madaktari wetu utasaidia chuo chetu pia” Dk. Shein alieleza.
Kwa hiyo alimueleza Profesa Stenner umuhimu wa kuwepo vievile ushirikiano kati ya Chuo cha Haukeland na Chuo Kikuu cha SUZA ili SUZA iweze kufaidika na utaalamu pamoja na uzoefu wa muda mrefu katika ufundishaji wa mdaktari na wataalamu wengine katika sekta ya afya.
Kwa upande wake Profesa Stenner ambaye alikuwa amefuatana na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa Bwana Jon Dahl alimueleza Rais kuwa ushirikiano baina ya taasisi unatoa matokeo mazuri ndio maana wao wameanzisha ushirkiano na Hospitali ya Mnazi Mmoja.
“Uzoefu unaonyesha ushirikiano wa kitaasisi unatoa matokeo bora zaidi na unakuwa na faida kubwa katika kujenga uwezo wa taasisi na ndio tunavyofanya sisi na hospitali ya Mnazi Mmoja” alaieleza Profesa Stenner.
Alifafanua kuwa msaada wanaoutoa kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja unagusa mahitaji halisi ya hospitali katika kutoa huduma kwa wagonjwa hivyo wanaamini wanatoa msaada wenye manufaa kwa watu wa Zanzibar.
0 Comments