6/recent/ticker-posts

Jumuiya za vijana za CCM na CUF kunani

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewatuhumu baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
 
Viongozi wanaotuhumiwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Jussa Ladhu, na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Aboubakari Khamis Bakari.
 
Tuhuma hizo zilitolewa jana  na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya Jumuia Maisara mjini Unguja.
 
Alisema viongozi hao wamekuwa na tabia ya kuwashambulia wenzao walio kwenye serikali hiyo ya umoja wa kitaifa  sambamba na kuvujisha siri za vikao mbalimbali.
 
Shaka alisema pia wamesikitishwa na tamko la Umoja wa Vijana wa CUF kuwataka wanachama wao waanze kufanya mazoezi ya viungo.
 
“Tamko la vijana wa CUF linaweza kuhatarisha uvunjifu wa amani na kuvuruga malengo ya kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sisi tunalikemea,” alisema.
 
Alibainisha kuwa kuundwa kwa serikali hiyo kulilenga kudumisha amani, utulivu na mshikamano baina ya wananchi wa visiwa hivyo pamoja na vyama vya CCM na CUF.
 
Shaka alimlaumu Maalim Seif kwa kukiri kuwa  mtiifu kwa Rais mstaafu Dk. Amani Karume huku akiahidi kushirikiana naye kusaka mamlaka kamili ya Zazibar katika  mfumo wa muungano badala ya Rais aliyemteua na kumuapisha kiapo cha kishesria Dk. Ali Mohamed Shein.
 
Shaka alisema tangu ianzishwe SUK vitendo vya uvunjifu wa amani pamoja na ubaguzi vimekithiri  kiasi cha kusababisha hali ya wasiwasi kwa wananchi.

Chanzo - Tanzania Daima

 
Na Mwandishi wetu
 
13th October 2013
 
Jumuiya ya vijana ya Chama cha Wananchi (CUF) imetoa tamko kali kuhusu matusi na kejeli dhidi ya viongozi wao yanayotolewa na Jumuiya ya Vijana wa CCM (Uvccm).
 
Tamko hilo limetolewa na Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Yussuf Kaiza Makame, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Vuga mjini hapa.
 
Alisema kukaa kimya haina maana hawana la kusema au wanaogopa bali CUF kinaendeshwa kwa misingi ya maadili na kidemokrasia.
 
Alisema jumuiya hiyo imechoshwa na kauli za matusi zinazotolewa hasa kwa Katibu Mkuu wa chama hicho ambae ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na sasa wamejipanga kikamilifu kokomesha vitendo hivyo kwa gharama yoyote.
 
Makamu mwenyekiti huyo alimtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kufahamu ana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi hivyo ameshindwa kukemea matusi yanayotolewa hadharani na CCM kwa kiongozi wao.
 
Alisema jumuiya ya vijana CUF inatambua kuwapo kwa kambi za makundi haramu ya vijana yalioandaliwa na CCM chini ya kiongozi mmoja wa serikali kwa lengo la kupiga kura zaidi ya mara moja katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 

Post a Comment

1 Comments

  1. Hawa ccm nacuf,wemona siku zimepita hawaja ifanyia kitu znz, sas wanajitia kulaumiana, kumbe lao moja kuvihujumu hivi visiwa,nusu na robo ya wakazi wake ni mafukara wakutupwa, na hakuna juhudi walioifanya na serekali yao yaumoja sas wanataka waanzishe zengwe ili wapate kuwahadaa wakazi, wasiulizwe ahadizao walizo waahidi wananch,

    ReplyDelete