6/recent/ticker-posts

Tuijenge Zanzibar yetu bila ya Ubaguzi, Zanzibar itajengwa na Wazanzibari wenyewe .

 
Na Ally Saleh
 
SIASA za uhasama na uchokozi zimerudi upya Zanzibar na kwa kipindi kifupi tu tokea zirudi tena hali imeanza kuwa tete. Ni wazi tunakoelekea siko; tunaelekea kubaya. Hili si ajabu kwa Zanzibar lakini halijawahi kuwa ni jambo linalokubalika, maana zikianza siasa kama hizi huishia matumizi ya nguvu na uhasama. Kila mtu hupata hasara, ingawa kwa kiasi kikubwa wapinzani ndio wanaoishia pabaya zaidi.
 
Viriri vimeanza kutumika kutoa kauli kali, za vitisho na hata za kibaguzi. Viriri vimetumika kutoa kauli za dharau, kebehi na za kutishia amani na mustakbali wa nchi yetu tuipendayo, Zanzibar.
Kama alivyotanabahisha mwenzangu katika uandishi Mohammed Ghassani kuwa hali hii imeanza kuwakumba hata ambao kwa kawaida huwa ni watu wa busara. Kidogo wakachukulika na siasa za jukwaani, wakateleza.
 
Ingawa wapo wanaoteleza kwa pande zote mbili za kisiasa, wapo pia ambao ni kawaida yao kutukana au ni maarufu kwa matusi na vijembe. Mashabiki wao huwa wanawashangiria ama kwa vicheko, makofi au kuwatia mori zaidi kwa misemo kama vile “ Wapashe baba” au “Toboa toboa” au hata “Chowea chowea.”
 
Miongoni mwa wanaoingia kwenye viriri wakifunga vibwebwe pia ni wanawake. Wao nao wamo. Tungetegemea hili lisitokee kwa vile tuna ustaarabu wetu wa wanawake wetu Wakizanzibari kuona haya, kujiheshimu na kujistahi.
 
Hata wakati wa siasa za uhasama wa kikweli kwenye miaka ya 50 na 60 wanawake walikuwa wakijizuia na walitumika zaidi kupoza kuliko kupuliza moto.
 
Tuliamua kwa makusudi kuzika siasa za chuki na uhasama kwa kuanzisha mfumo wa maridhiano chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya wanasiasa wakuu katika mivutano na misuguano, Maalim Seif Shariff Hamad na Sheikh Amani Karume kusema na nyoyo zao walipoona hatari ya nchi inakoelekea.
 
Ndipo katika kutimiza dhamira hiyo ya Novemba 5, 2009 pakafanywa Kura ya Maoni Agosti 31, 2010 iliyothibitisha kuwa asilimia 66.4 ya Wazanzibari walichagua kuachana na siasa za uhasama ingawa bado wakitaka siasa za vyama vingi na ushindani ziendelee kwa ajili ya uwepo wa demokrasia ambayo imekua hapa kwetu.
 
Si vyema, si haki, si halali kabisa kwa mtu yoyote kupuuza maamuzi hayo ya thuluthi mbili ya Wazanzibari. Haikubaliki, haiwezekani na asiachiwe mtu yoyote yule kudharau, kubeza na kuyapiga buti maamuzi hayo.
 
Serikali ya Umoja wa Kitaifa imetuokoa na mengi tangu iundwe. Tumeona jinsi kwa mara ya kwanza kwa Uchaguzi Mkuu ulivyofanywa kwa salama na amani bila ya hata mtu kufinywa.
 
Niseme wazi hapa kuwa wafaidika wa kubwa wa utulivu huu ni wananchi ambao wameamua kuwa upande wa siasa za upinzani ambao kwa miaka tokea 1992 zilipoanza siasa za vyama vingi mpaka 2009 ndio waliopigwa, kuteswa, kuonewa na kunyimwa kila aina ya haki.
 
Wale wa upande wa chama ambacho kimekuwa madarakani hawajui shida ya kuwa mpinzani nchi hii kwa sababu toka 1964 hadi 1992 na kutoka 1992 mpaka 2009 ni wachache mno kati yao waliofinywa ukucha, waliobaguliwa, waliosingiziwa kesi, waliofirigiswa, kukoseshwa cheo, kubaguliwa katika masomo na kufanyiwa kila aina ya idhlali.
 
Hadithi ya madhila haiwezi kabisa kuhadithiwa na yoyote ambaye amekuwa mwanachama wa CCM. Kwa hivyo, kwa fikra zangu ni rahisi kwao kutokuuona umuhimu wa kulinda amani na umoja wa kitaifa. Sisemi kuwa walio chama cha upinzani hawawezi kuwa pia ni waharibifu wa amani lakini wa CCM ndio waliobobea.
 
Kama nilivyotangulia kusema pande zote mbili zina wajibu wa kuishika, kuienzi na kuibembeleza amani maana hata katika hiyo miaka ya 1964-1992 na 1992 mpaka 2009 Serikali haikuweza kupiga hatua za wazi na jumuishi za maendeleo maana siasa haikuwa imekaa sawa.
 
Ingawa mimi binafsi siridhiki na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao unaishia kileleni bila ya kushuka kwenye matawi na mizizi, lakini naona faida kubwa sana ya kuwepo na kuendelezwa kwa mfumo huo. Pengine tunawajibika tuupe nguvu na mashiko zaidi tu.
 
Kwa hivyo wakati tukipanda viriri vya siasa kufanya siasa ni lazima tutashindana kwa hoja, tutakosoana kwa jazba, tutaonyeshana vidole na kushutumiana wakati mwengine, maana hakuna kabisa siasa za kimyakimya au zisizo na nguvu na mikiki.
 
Lakini kabisa, tena kabisa isifike tukataka, au tukapenda kurudi katika siasa za chuki na uhasama kwa sababu hakuna atayefaidika. Tukumbuke pia hata hao wapinzani waliokuwa wakionewa muda wote hawatakubali kuendelea kuonewa sawa na wale ambao wamekuwa wakifaidi nguvu na fursa za kutawala wajuwe kuwa haki ya kutawala ni ya wote.
 
Fikra zangu basi pamoja na yote isifike kabisa tena kabisa kwa yoyote yule, narudia kwa yoyote yule kusema au kutamani kuwa jahazi la Zanzibar litote na tugawane mbao, maana anayesema hivyo au anayeashiria kwa kauli zake au vitendo ajue kutota Zanzibar ni kuipasua Zanzibar tuipendayo, na hatujui itapasuka vipande vingapi.
 
Tushindane kwa hoja, nguvu na ujanja lakini tusifanye chochote ambacho kitaipelekea Zanzibar kutota maana ikitota ni hasara kwetu tuliopo sasa na vizazi vijavyo. Wallahi, haki ya Mungu tupate faida gani Zanzibarikitota.
 
Tusimruhusu, tusimkubalie yoyote kutamka hivyo na tumwandame na kumwelewesha kuwa tukitota na janga, na watu walisema mchuma janga hula na wa kwao

Post a Comment

4 Comments

  1. Nahsukuru muandishi kw kuliona hili, lakini tunajambo la kujifunza, kwenye hii serekali ya umoja wakitaifa, nalo ni hii amani, ya kiuongo, tulioyonayo, sasa utaona upande mmoja ukishutumu upande wmwengine kama haupo ndani suk, hilini jambo laajabu, ndio kutafuta uhasama wakusudi, haw, vingozi,wasuk, ilikuwa watawambie hatima ya znz ,yetu sikulumbana,tunao, kulumbana kwao ni kama geresha uli waznz, wasiwaulize ahadi walizotoa wakati wakampen, wanafanya hivi kwa malengo yao, sikweli kama wana ugovi, wanachotaka kufanya nikulinda mslahi yao binapsi tumeona mawaziri pande zote2 niwezina wafujaji wa mali za znz, na, tusha wasika viongozi wa kitaifa wakisema ndaina ya serekali wapo kitukimoja kuwkanda miza wakulima na wakwezi, sas humchezo waotumeujua, uchaguzi una karibia wanapotezalengo watu

    ReplyDelete
  2. Hii ni mada nzuri.I hope wanaofanya matendo haya watatafakari zaidi. Unajua tatizo ni kuwa hawa jamaa wanahisi kuwa hakuna polisi anaeweza kuwakamata na hakuna kiongozi wa juu ambae anaweza kuwakemea.

    ReplyDelete
  3. Hili jambo lililoandikwa hapa ni kampeni tu za kuifagilia CUF na wála sioni hoja madhubuti yenye maslahi ya wengi. Hoja ni ubadhilifu uliojaa serikalini. Mbona nyinyi mnaojifanya magwiji wa kuandika hamsemi haya? Ubadhilifu umeiua na unaendelea kuiua Zanzibar na wala sio matusi.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Huu ubadhirifu haukuwepo siku zote mpaka ilipokuja serikali ya umoja wa kitaifa? Naona hata mheshimiwa Shamsu anasema hili wakati yeye pia alikuwa katika serikali. Sasa ubadhirifu ulianza lini?

      Delete