Habari za Punde

WALIOCHANA MSWADA NI WAHUNI - WAZIRI SAMIA

Basil Msongo , Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan amesema, watu waliochana muswada wa sheria itakayosimamia mchakato wa kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania ni wahuni.

Waziri Samia amesema, kitendo kilichofanywa Zanzibar si tabia ya Wazanzibari na kwamba, waliofanya hivyo ni kundi la wahuni.

“Kwa hiyo wamejumuika, wamekuja kufanya uhuni wao pale” amesema Waziri huyo wakati anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge mjini Dodoma.

“Ile isichukuliwe kuwa ni tabia ya Wazanzibari kwa kuwa wamesema vile” amesema na akabainisha kuwa, kilichotokea ni tofauti ya mawazo na mitazamo miongoni mwa wananchi.

Waziri Samia ameyasema hayo wakati anazungumzia mafanikio na changamoto za muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakati huu unapokaribia kutimiza miaka 47.

Amesema, Muungano huo ni imara lakini kuna vikwazo katika utekelezaji wa Sheria ya Muungano.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, viongozi wa Zanzibar na Tanzania Bara wamekubaliana kuwasilisha miswada Katika Bunge na Baraza la Wawakilishi Oktoba mwaka huu ili kuondoa utata wa kisheria uliopo kati ya pande hizo.

“Kuwa na mfumo tofauti wa sheria kwa pande mbili za muungano hukwamisha utekelezaj i wa baadhi ya maamuzi yanayofikiwa katika kutatua vikwazo vya muungano, mfano katika masuala ya usajili wa magari n.k” amesema.

Amesema, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikishirikiana kuondoa vikwazo ili muungano uendelee kuwa imara na uwe na faida kwa wananchi wa pande zote.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, tangu mwaka 2006 vimefanyika vikao sita vya kamati ya pamoja ya Serikali ya Muungano na SMZ, na kwamba, vikao hivyo vilitanguliwa na vikao vya mawaziri, makatibu wakuu na wataalamu wa kisekta kutoka serikali zote mbili.

Amesema, hoja 13 ziliwasilishwa na kujadiliwa, mbili zimetatuliwa, zikaandaliwa hati za makubaliano, mawaziri wa serikali zote mbili walizisaini Juni 2 mwaka jana mjini Zanzibar.

Samia amesema, hoja nne zimepatiwa ufumbuzi ambazo ni mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada kutoka nje, misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF, uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi, na malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.

Amezitaja hoja zilizo katika hatua mbalimbali za kutafutiwa ufumbuzi kuwa ni ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili, uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu, ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje, na ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.

Hoja nyingine ni mgawanyo wa mapato yanayotokana na faida Benki Kuu na hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki.

Amesema, hoja nyingine inayotafutiwa ufumbuzi ni kodi nyinginezo ikiwemo Kodi ya Mapato, Kodi ya mapato inayozuiwa na usajili wa vyombo vya moto yakiwemo magari na pikipiki.

Chanzo: Habari Leo

2 comments:

  1. Bi samia naona unaota mbawa siku hizi ...hunoni kilichowqafika kina BEN ALI na MUBARAK kwa ajili ya udikteta wao ? wacha watu watoe maoni yao kwani hicho kilichochanwa sio kitabu cha Allah,hapo kilipochanwa hukusema chochote

    unamjua alochana huo mswada mapaka umwite muhuni ? kati yako na yake yeye ni nani ana shepu ya kihuni ? Ulimi umeponza kichwa........wazenji weshajua kuwa wewe ni maslahi tu na hupo kwa ajili ya kuwateta wao ili wakwamuke katika janga hili la huu muungano.

    mtizame Shamhuna kwa sasa anaonyesha kujirekebisha lakini bado mupo vidudu watu wengine ...........

    ReplyDelete
  2. Asalaam aleykum!
    mimi binafsi nakubaliana na bi Samia kwamba kitendo cha kuchana muswada ambao umeletwa kwa ajili ya kuujadili ni kitendo cha kihuni hata kingefanywa na nani.Madhumuni yakufanywa mikutano ni watu kutoa maoni yao juu hicho kilichoandikwa,kama kizuri ama kibaya na hakuna mtu alielazimishwa atoe mawazo ya aina fulani . Tume ipo kwa ajili ya kukushana hayo maoni sasa inanisikitisha kuona kiongozi wa dini anafanya kitendo kama kile.Kitendo ambacho kilitakiwa kufanywa na mtu ambae hana elimu hata kidogo wala maarifa au busara. Ni kitendo cha kishenzi ambacho kinarudisha nyuma ustaarabu wa kizanzibari haswa katika wakati huu ambao wazanzibari wako wamoja katika serikali ya umoja wa kitaifa.Mimi naunga mkono kabisa na wachangiaji ya kwamba mswaada unamatatizo ya kimsingi ambayo lazima yarekebishwe lakini sio hatua iliochukuliwa na huyo anaitwa Ustadh .Wastaarabu walitoa mawazo bwawani na haile salesie mpaka mtu unapata mafunzo na unasoma mengi usiyoyajua.Kwake yeye tumesoma nini zaidi ya ujinga na uhuni?sidhani kama ni busara wala uungwana Kufanya alivyofanya?.
    Ustadh alitakiwa ausome huo mswaada kifungu hadi kifungu na aukosoewe na atoe mapendekezo yake kama ya kujenga ama kubomowa.Mimi binafsi nashaangaa kwanini mpaka leo jeshi la polisi hawajamkamata kwa kutaka kuhatarisha amani na makosa mengine na kumshitaki mahakamani .
    kuchana mswada sio kutoa maoni ni uhuni,ujinga hata angefanya nani basi angekuwa katika kundi analosema Bi samia.Liite pauro ,pauro hakuna jina jengine!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.