Habari za Punde

ZAIDI YA 5.4 BILIONI ZATUMIKA TASAF PEMBA

Na Youssuf Hamad, Pemba

JUMLA ya shilingi 5,474,466,601 bilioni, zimetumiwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF ii) kwa ajili ya kutekeleza miradi 348 ya wananchi katika wilaya nne kisiwani Pemba.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi iliyofadhiliwa na mfuko huo, kwa ujumbe wa benki ya dunia, Mratibu wa TASAF Pemba, Issa Juma Ali amesema kati ya fedha hizo TASAF imechangia shilingi 5,003,856,401 bilioni na wananchi wamechangia shilingi 470,610,200 milioni.

Mratib Issa ameuambia ujumbe huo wa benki ya dunia kwamba miradi hiyo 348 ya wananchi imetekelezwa katika wilaya zote nne za Pemba, ambapo wilaya ya Mkoani miradi 87, Chake Chake miradi 85, wilaya ya Wete miradi 88 na wilaya ya Micheweni miradi 88 na kunufaisha zaidi ya wananchi 192,134.

“Miradi hii ilitekelezwa kwa kuangalia kipaumbele cha jamii yenyewe kwa kupitia mikutano ya wazi ambayo huwashirikisha wanajamii wote” alifafanua Issa.

Mratib huyo wa TASAF Pemba ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na miradi ya elimu, nyumba za madaktari, ujenzi wa bara bara kwa kiwango cha changarawe, miradi ya mazingira, kilimo cha umwagiliaji maji, ufugaji wa mbuzi na ng’ombe wa maziwa, vinu vya kisasa vya nafaka na upandaji wa mikoko.

Miradi mengine ni kilimo cha mboga mboga, elimu ya ukimwi, ujenzi wa masoko ya samaki, kuendeleza maeneo ya kihistoria, ufugaji wa samaki, uvuvi, kilimo cha mwani na uzalishaji wa chumvi.

Mratib Issa aliema kuwa miradi ya maji safi na salama kwa ujumla wake imetumia shilingi 434,997,936 milioni, ambapo miradi ya elimu imegharimu shilingi 322,653,989 milioni, huku miradi ya afya na ujenzi wa bara bara ilitumia shilingi 313,003,439 milioni na miradi ya michirizi ya maji machafu imetumia shilingi 69,719,930 milioni,.

Alisema kuwa mingine ni miradi ya umwagiliaji maji iliyotumia shilingi 215,799,046 milioni, ambapo miradi ya ufugaji imetumia shilingi 1,009,653,719 minioni huku vinu vya kusagia nafaka vimetumia shilingi 130,812,895 milioni na upandaji wa mikoko umetumia shilingi 305,844,895 milioni ambapo elimu ya ukimwi ikitumia shilingi 274,001,731 milioni na kilimo cha mboga mboga kimetumia shilingi 20,000,000 milioni.

Miradi mengine ni ujenzi wa masoko umetumia shilingi 113,244,008 milioni, huku sehemu za kihistoria zikitumia zikitumia 129,166,690 milioni na miradi ya uvuvi kwa ujumla wake imetumia shilingi 1,478,865,950 milioni.

“kwa kweli azma ya serikali kwa kiasi kikubwa imefikiwa kwani fedha hizi zaidi ya shilingi bilioni tano, zimekwenda kwa wananchi kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kweli wameweza kupunguza umasikini kwa jamii ya Pemba”alisema Issa.

Akizungumzia changamoto wakati wa kutekeleza miradi hiyo, mratib wa TASAF Pemba, amesema taaluma ndogo ya manunizi miongoni mwa kamati, usafiri kwa wataalamu wa kilimo kwenda katika miradi na masoko madogo kwa bidha zinazozalishwa ni miongoni mwa vikwazo kwa maendeleo ya miradi hiyo.

Nae kiongozi wa ujumbe huo wa bank ya dunia Abella Diallo amesifu juhudi zinazochukuliwa na mfuko huo katika usimamizi na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na bank yake.

Alisema bank ya dunia imeridhishwa na utekelezaji huo hasa katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji maji, kwani miradi hiyo inakwenda sambamba na utekelezaji wa sera ya serekali ya ya tanzani ya kilimo kwanza.

“Benki ya dunia inaamini kwamba unapowawezesha wakulima katika kilimo cha umwagiliaji maji, unawafanya walime zaidi na hivyo wataongeza uzalishaji na hatimaye kupata akiba ya chakula” alifafanua Diallo.

Mapema ujumbe huo ulionana na Katibu mkuu ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Khalid Salim Mohammed ambapo aliuambia ujumbe huo wa benki ya dunia kwamba miradi ya TASAF hapa Zanzibar imefanikiwa vizuri ukilinganisha na miradi mingine, inayofadhiliwa na benki hiyo.

Hata hivyo Dk. Khalid alisema kuwa ucheleweshaji wa fedha za miradi kutoka benki hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokamilika miradi kwa wakati kutokana na mfumuko wa bei za bidhaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.