Habari za Punde

LENGO LA KUIPANDISHA DARAJA HOSPITALI MAKUNDUCHI LITAFIKIWA - DK SHEIN

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa lengo la kuipandisha daraja Hospitali ya Makunduchi  kufikia hadhi ya Hospitali ya Wilaya litafikiwa.

Dk. Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Makunduchi, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzungumza na viongozi wa CCM,  Unguja na Pemba ambapo tayari amemaliza kuzungumza na viongozi wa Wilaya zote za Unguja.

Katika hotuba yake kwa viongozi hao Dk. Shein alisema kuwa serikali ina mpango wa kuifanya hospitali hiyo kuwa ya Wilaya kwani tayari hadhi inayotakiwa imeshafikiwa na kubwa lilobaki hivi sasa ni kuongeza vifaa pamoja na majengo ya ziada.

Akitoa maelezo yake kutokana na ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika mikoa mitano ya Zanzibar ukiwemo Mkoa huo wa Kusini Dk. Shein alisema aliwaeleza viongozi hao wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja, kuwa hatua hiyo inatokana na kasi ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo imeanza kutekelezwa kwa kasi.

Kutokana na hatua hiyo aliwataka viongozi hao wa CCM Wilaya wazidishe mashirikiano na mshikamano miongoni mwao kwa azma ya kufikia malengo yaliowekwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM  kwenye sekta zote za maendeleo.

Akieleza juu ya azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuiimarisha sekta ya afya na kuwapeleka huduma hiyo karibu na wananchi, Dk. Shein alisema kuwa hospitali ya Makunduchi inayoendeshwa kwa mashirikiano na mradi wa ‘Health Imrovement Project Zanzibar’ tayari imeshawekewa mikakati maalum ya kuiimarisha.

Katika hospitali hiyo Dk. Shein alisema kuwa huduma mbali mbali zimeanza kutolewa zikiwemo huduma za akina mamam na watoto, upasuaji, X-ray, huduma za utoaji meno, ‘Utra sound’, “oxygen concentrator” na huduma  nyenginezo.

Pia, Dk. Shein aliipongeza kwa mara nyengine tena Halmashauri ya Wilaya ya Kusini kwa kuongeza kukusanya mapato kutoka milioni 42 hadi kufikia milioni 64 ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wachapa kazi na wenye ujuzi.

Akieleza juu ya tatizo la ardhi ambalo pia, limekuwa ni tatizo sugu katika Wilaya hiyo alirejea kauli yake ya kuwataka viongozi wa Mkoa, Wilaya, Wizara, Wadi na Shehia kuyatatua wenyewe matatizo hayo na baada ya hapo ndio wapeleke taarifa ngazi za juu.

Dk. Shein hakusita kuwaeleza viongozi hao wa CCM kuwa ahadi yake aliyoahidi ya kuyaangalia maslahi ya wafanyakazi wa serikali ili yawe bora kidogo kuwa ahadi hiyo ipo pale pale na utekelezaji wake utaanza mwaka huu wa fedha.

Alisema kuwa mbali ya hatua hizo za mishahara pia, serikali imeandaa taratibu za kupeana daraja, taratibu za kupeana maongezeko pamoja na kuuangalia utumishi wa daraja kwa wafanyakazi wa serikali ili wafanye kazi kwa ari.

Pia,  Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa kwa wale wanaoondoka nchini kwenda kufanya kazi nje ya nchi serikali itafanya utaratibu ili wabakie hapa hapa nyumbani kwa lengo la kuitumikia nchi yao.

Kwa upande wa sekta ya elimu Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa ujenzi wa skuli mpya za sekondari za Wilaya unaendelea kwa kasi kubwa kwani ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ilieleza kuwa skuli hizo zitajengwa ndani ya kipindi cha miaka mitano na badala yake zimejengwa kwa  mwaka mmoja.

Dk. Shein alisema kuwa skuli hizo ambazo zinajengwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia, kila moja inagharimu kati ya shilinmgi za Kitanzania Bilioni 1.4 hadi Bilioni 1.6 na kueleza kuwa skuli mbili kati ya hizo zinajengwa kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu ‘BADEA’ mbazo ni skuli za Kibuteni na Mkanyageni.

Pia, Dk. Shein aliwahakikishia wanananchi wa Makunduchi pamoja na Majimbo mengine yaliyomo katika Wilaya hiyo kuwa serikali imo mbioni kulitatua tatizo la maji, ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata  huduma hiyo kwa uhakika zaidi.

Aidha, aliwaeleza viongozi hao wa CCM kuwa wana kila sababu ya kuendeleza  mashirikiano yao kwani hiyo ni nguzo pekee ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Shein pia, aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa mashirikiano kati yao na wanachama wa ngazi za chini kwani nao wana umuhimu mkubwa katika kukiimarisha chama hicho kwani pia, walichangia kuwapa uongozi viongozi hao.

Pamoja na hayo Dk. Shein aliwataka viongozi hao kujenga ari ya kuchangia kwani utamaduni huo umepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka ya nyuma.

Kwa upande wa sekta ya kilimo Dk. Shein aliahidi kuwa serikali yake itafanya kila juhudi katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wakulima wakiwemo wakulima wa mpunga, mbogamboga na matunda.

Kwa upande wa mfumko wa bei, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa hilo ni tatizo la dunia nzima na si la Zanzibar peke yake lakini hata hivyo serikali yao inafanya juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo pamoja na mipango ya kuweka hakiba ya chakula. 

Dk. Shein alieleza kuwa lengo kubwa katika kipindi kifupi kijamcho ni kuzaalisha kwa kiasi kikubwa mpunga na kufikia kuzalisha tani  40 elfu hapa nchini na lengo ni kulima mpunga hapa hapa Zanzibar kwani matumizi ya mchele ni tani 80 lakini uzalishaji wa chakula hicho unaozalishwa hapa Zanzibar ni tani 14 tu.

Aliwaeleza vijana kuwa serikali yao imo katika mipango kabambe ya kuwahakikisha nao wanafaidika na juhudi hizo zinazochukuliwa kwa maslahi ya maisha yao.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alitoa pongezi kwa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kwa ziara zake za kwenda kuzungumza na viongozi wa CCM na kueleza kuwa Wilaya hiyo pamoja na Mkoa mzima wa Kusini hawana mzaha katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Akitoa shukurani kwa niaba ya viongozi hao wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja, Mlezi wa chama hicho Mkoa huo Issa Baharia alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuwaeleza ukweli wananchi na viongozi wa CCM  juu ya mfumko wa bei za bidhaa, vikiwemo vyakula ambavyo asilimia kubwa hununuliwa nje ya nchi.

Alisema kuwa bei ya bidhaa, vikiwemo vyakula zimepanda ambazo zimechangiwa zaidi na kupanda kwa kiasi kikubwa  kwa bei ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa hizo kutoka ngambo. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.