Habari za Punde

KUCHOMWA BAA ZA VILEVI NINI TATIZO?

Zamani kulikuwa na ngoma ya kindumbwendumbwe. Hii ikipita mitaani basi kuna jambo. Jambo lenyewe huwa ni zito kiasi cha kuwafanya majirani wote kutoka na kutaka kuona ni nani huyo aliyepigiwa kindumbwendumbwe?


‘Kindumbwendumbwe charia, kikojozi kakojoa na nguo kaitia moto’ ni sehemu tu ya wimbo huu ambao mtu mwenye tabia ya kukojoa kitandani hupitishwa mitaani na kuadhirishwa. Hapigwi bakora wala haguswi bali tu uso wake hupakwa masizi au mkaa na kuaibishwa. Naam ilikuwa dawa tosha kwani anajua kwamba akikojoa tu taazira hiyoo.... Akipita tu mtaani kila mtu anamjua kikojozi yulee...

Leo hii Kikojozi wa aina hii akiitwa kikojozi basi kwake ni sifa na aibu tena. Ukijaribu kumleta mtaani na kumuaibisha basi kwake yeye huwa ni sifa na si aibu.

Kilichonisikuma kuandika ujumbe huu ni matukio ya kuchomwa moto kwa Baa yaliyotokea katika mwezi huu 
mtukufu wa Ramadhaan ambao unafikia tamati, Na InshaAllah Mla atukubalie Swaumu zetu na ibada zetu.

Nikiunganisha na matukio ya kuchomwa moto mabanda ya wafanya biashara Mangapwani miezi kadhaa iliyopita kuna jambo hunijia katika fikra zangu kwamba ima vyombo vya Dola vimeshindwa kufanya kazi ndiyo maana Wananchi hujichukulia sheria mkononi au Wananchi wametambua nini wajibu kwa jamii na hivyo kuutekeleza bila ya kujali madhara na athari za matendo yao. Sina jibu kwa hilo.

Ila matukio haya hayaji kwa sudfa au bahati na mazalio ya kuambiwa ufagie nyumba na kisha badala ya uchafu kuutupa nje unaupeleka chini ya zulia na hufika wakati uchafu ule unaonekana nje pepepe. Na hapo ndipo tulipofikia ila wenye dhamana wanalikanusha hilo na kudhani hawa ni watu wachache tu ambao wanataka kuharibu amani ya nchi.

Kuna mtu aliwahi kutoa maoni kwamba nchi ya Zanzibar inatawaliwa na utawala wa Sheria. Hivyo tuiachie Sheria ichukue mkondo wake na si kujichukulia Sheria mkononi. Hii ni sawa kabisa endapo tu huo utawala wa Sheria unatekelezwa ipasavyo na kila mwenye dhamana yake anaitekeleza kwa mujibu wa Sheria. Ama ikiwa upande uliopewa dhamana unapindisha Sheria huku ukitarajia mwengine anyamaze tu ndiyo yalilyotufikisha hapa.

Vibali na leseni hutolewa bila ya kujali wananchi waathirika ambapo Baa huwepo katika maeneo ya watu wakati Sheria hairuhusu hivyo. Vyombo vya Dola kama Polisi vinavyoendekeza rushwa kuliko kutawala kisheria ni matunda ya aina ya watu hawa kuamua wakati umefika nasi tuamue.

Leo hatuwezi kumuadhiri mlevi kwa kindumbwendumbwe, wala mteja kwa kumpaka masizi , Mtoa leseni keshapata chake hamjali mwananchi na Polisi ndiye wa kwanza anayekuja kumtaarifu muuza Unga kama kwamba kesho ‘tunakuja’ akiondoka na chake akimjali muuza unga kuliko muathirika. Je  kisa ni mfumo, shida, dhiki au ulimbukeni???

1 comment:

  1. Kaka ahsante kwa mada yako nzuri, na nafikiri kwa kutumia njia ya majadiliano kupitia blog hii tunaweza kujenga zanzibar mpya,lkn pia tusisahau kuwahamasisha vijana kutumia blog hii.tukija kwenye mda yetu,mm nadhani vyombo vya dola vinapaswa kulaumiwa. Sina hakika na suala la rushwa lkn lile la uzembe wa kutokuwajibika liko wazi! tuchukuwe mfano wa miaka 15 iliyopita, wakati wa mikiki mikiki ya siasa,polisi waliweza kufichua na kuzuia uhalifu wote uliohusiana na siasa, walikua hawalali,mpaka kieleweke! hata ukitoa rushwa walikua hawapokei!Leo imekuwaje kwa watu wanao hatarisha umoja wa taifa letu na ku turnish image ya zanzibar huko nje? wanaachwa scort free!inskitisha!. lkn pamoja na yote tusiruhusu mt yeyote kuchukua sheria mikononi,kwani tuna wasiwasi mentality za aina hii zikianza hazitaishia hapo!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.