Habari za Punde

USHIRIKISHWAJI SEKTA BINAFSI - NJIA YA KUHARAKISHA MAENDELEO

Othman Khamis Ame, Washington DC

Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika miradi na Taasisi za Kijamii ndio njia pekee ya kuharakisha Maendeleo ya Wana Jamii popote pale hasa ikizingatiwa zaidi mfumo wa Utandawazi uliopo ulimwenguni hivi sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Mtaalamu muandamizi wa Maendeleo ya Kimataifa Profesa Luis Rodriguez pamoja na Bibi Beatrice Biha anayehusika na Mpango wa Elimu wanaotoka Jumuiya ya Kijamii inayojishughulisha na masuala ya Elimu na Afya Nchini Marekani wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Ubalozi wa Tanzania Mjini Washington DC akianza ziara yake ya siku nane Nchini humo.


Profesa luis na Bibi Beatrice walisema mfumo wa sasa wa utandawazi kwa kiasi kikubwa umesaidia kukua kwa uchumi kwa mataifa Makubwa jambo ambalo linaweza kusaidia endapo litatekelezwa na mataifa machanga kama Zanzibar.

Wawakilishi hao wa Jumuiya ya Kijamii inayojishughulisha na Masuala ya Elimu na Afya wamefahamisha kwamba Liberia ambayo imefanikiwa kutekeleza mpango wa Elimu kupitia Jumuiya hiyo imepata mabadiliko makubwa ndani ya kipindi cha miaka 14 iliyopita.

Wamesema Jumuiya yao inaangalia uwezekano wa kufanya kazi pamoja na Jumuiya za Elimu za Zanzibar kwa lengo la kusaidia harakati hizo.

" Tunahitaji kuona elimu ya Teknolojia inaingia hata kwa familia za wananchi wenye kipato cha chini. Hii itakuwa changamoto kwa familia hizo kuweza kujipunguzia ukali wa maisha". Alisema Profesa Luis Rodriguez.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajipanga kuhakikisha kuona Elimu ya Juu inapewa nafasi pekee.
Balozi Seif alisema lengo kuu la mipango hiyo ni kuongeza vyuo Vikuu ikilengwa zaidi vile vya sayansi ili kwenda sambamba na Mabadiliko yaliyopo Duniani ya Sayansi na Teknolojia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Jumuiya hiyo kwa kuonyesha hamu ya kuitembelea Zanzibar kuona jinsi gani inaweza kushirikiana katika kuupa msukumo mpango huo.

Wakati huo huo akihojiwa na changamoto yetu bloc. com ya Mjini Washington mara baada ya Tafrija fupi aliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania Mjini humo yeye na Ujumbe wake Balozi seif alisema nia ya ziara yake ni Kuitangaza Zanzibar kwa Mashirika na Taasisi za Marekani kuweka kuwekeza Vitega Uchumi vyao Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif alisema Miundo mbinu iliyopo hivi sasa Zanzibar inatoa fursa nzuri kwa wawekezaji hao kuweka vitega uchumi vyao kwa lengo la kujipatia mapato na kuisaidia Serikali kupunguza mzigo wa ajira hasa kwa vijana wanaomaliza skuli.

" Wapo vijana wengi wa form 1V na Form V1 hawana kazi. Hivyo uanzishwaji wa Viwanda na Miradi ya uwekezaji inaweza kusaidia kupunguza wimbi hilo ".Alisema Balozi Seif.

Mapema Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiislamu Mjini Washington DC Bwana Iddi Sandari amemkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mchango wa Dolla za Kimarekani 4,000 kusaidia Mchango wa Maafa Kufuatia Janga la Ajali ya Meli ya M.V Spice Islanders iliyotokea mwezi Septemba mwaka huu.

Bwa iddi amesema Maafa hayo wao kama Jamii imewagusa na wamefikia uwamuzi wa kuungana na Wazanzibari katika msiba huo mzito uliovikumba Visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif ameushukuru uongozi wa Jumuiya hiyo kwa kuguswa kwao na Janga hilo na kuelezea haraja yake kuona kwamba hata jumui za nje ya nchi zimeguswa na msiba huo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.