Habari za Punde

BALOZI SEIF ATEMBELEA KITUO CHA TELEVISHENI KARUME HOUSE

Mfanyakazi Wa Shirika La Utangazaji Zanzibar { Televisheni } Abdullhakim Haji Jecha Akiwa Miongoni Mwa Watendaji Wa Kituo Hicho Wakielezea Matatizo Wanayopambana Nayo Kituoni Hapo Mbele Ya Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Aliyetembelea Kituo Hicho
Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Akizungumza Na Viongozi Pamoja Na Baadhi Ya Wafanyakazi Wa Kituo Cha Televisheni Cha Shirika La Utangazaji Zanzibar Kiliopo Karume House.

Mkurugenzi Mkuu Wa Shirika La Utangazaji Zanzibar { Zbc } Ndugu Hassan Abdulla Mitawi Akimpatia Maelezo Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Aliyefika Karume House Kuangalia Utendaji Kazi Wa Kituo Cha Matangazo Ya Televisheni Ya Zbc.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekumbusha kwamba mafanikio ya kazi popote pale hupatikana na kuongezeka iwapo suala la kuheshimiana litapewa nafasi kubwa kati ya Viongozi na Watendaji wao.

Balozi Seif ametoa kumbusho hilo alipofanya ziara fupi ya kuangalia utendaji wa kazi na matatizo yanayokikabili Kituo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {Televisheni} Karume House Mjini Zanzibar.

Alisema utaratibu wa kujumuishwa kwa mawazo ya watendaji wadogo hata kama Dereva au Muhudumu unapelekea kuleta ufanisi wa haraka wa kazi katika Taasisi yoyote ile.


Balozi Seif alifahamisha kwamba nidhamu ya kazi lazima izingatiwe na kutekelezwa vyema vyenginevyo kazi inaweza kuharibika kama suala la dharau litaendelezwa miongoni mwa Watendaji na Viongozi.

“ Hakuna kitu ninachokichukia na kunikera ndani ya nafsi yangu kama tabia ya Wafanyakazi Hasa Viongozi kuwa na hulka ya kudhalilishana. Hii tabia ya Intimidation inanikera kweli kweli ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Aliwataka watendaji hao wa Kituo cha Matangazo ya Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } kuendelea kufanya kazi zao kwa uzalendo ili kuondoa mapungufu yaliyomo ndani ya uwezo wao.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali itajitahidi kuona yale yanayorekebishika yanatekelezwa mara moja kwa lengo la kukirejeshea hadi yake kituo hicho cha mwanzo cha rangi Barani Afrika.

“ Ni vyema Tv yetu ikarejea kama zamani na iwapo kama upo upungufu wa Wataalamu Suala hilo lishughulikiwe na Serikali ”. Alishauri Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Wakitoa malalamiko yao Baadhi ya Watendaji wa Kituo hicho cha matangazo ya Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } wameelezea kuzingatiwa kwa ufinyu wa Bajeti ya Vipindi ya kituo hicho.

Wamesema Bajeti hiyo haikidhi mahitaji halisi ya Utayarishaji vipindi na kulazimika kutumia Vipindi vingi vya kununua na vile vya kigeni ambavyo mara nyingi vinakiuka maadili na Utamaduni.

Kuhusu suala la Maposho ya ongezeko la muda wa kazi Watendaji hao wamesema jambo hilo ni ndoto na limekuwa likirejesha nyuma utendaji kazi wao wa kila siku.

Hata hivyo wameomba kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kujiweka tayari na mabadiliko ya mfumo wa kisasa wa Matangazo ya Digital unaotarajiwa kuanza rasmi mwaka 2015 Ulimwenguni kote.

Mapema akimkaguza Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika baadhi ya sehemu za Kituo hicho zikiwemo zile za Mitambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } Nd. Hassan Abdulla Mitawi alisema hatua za awali zimeshachukuliwa na kituo hicho za kuelekea kwenye mfumo wa Digital.

Hata hivyo Nd. Mitawi alimueleza Balozi Seif kwamba Kituo hicho bado kinakabiliwa na changa moto ya Vifaa na Mafunzo ya Watendaji wake ili kujiweka tayari na mfumo huo mpya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif miongoni mwa sehemu alizobahatika kuzitembelea kituoni hapo ni pamoja na Chumba cha kurushia Matangazo { Master Contol Room } , Studio kubwa pamoja na Library.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/12/2011.

2 comments:

  1. Asalamu alaykum,
    Wafanyakazi hao wa TVZ wanawasikiliza viongozi wao kwa shingo upande, hii nafikiria kuwa hakuna maslahi yoyote waliyopewa hapo na viongozi hao, bali ni maneno matupu tu.
    Kweli inatia huruma sana . Poleni sana wana TVZ.

    ReplyDelete
  2. Serikali, haikatai kuwapa maslahi zaidi lakini hali hairuhusu. Vyombo vyetu vinategemea ruzuku ya serikali pekee ili vijiendeshe, vimeshindwa hata kubuni mikakati ya kibiashara ili kujisaidia.
    Baya zaidi TVZ ndio televisheni kongwe zaidi hapa nchini lakini bado inaendeshwa kienyeji, kiasi kwamba hata wafanyakazi wake.. maskini, hawawezi kuajiriwa hata na TV binafsi ambazo zinaonekana kufanya vizuri. Ukitoa MARIN HASSAN. ambae amekua ICON ya vipaji vya wazenj katika fani ya utangazaji. Watu huona bora kutrain vijana wapya kuwa watangazaji wa TV kuliko kuja ZNZ, ambako kuna uzoefu wa kumwaga!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.