Habari za Punde

Makubwa Yaibuka Muswada wa Mafao ya Viongozi Z`bar

Na Mwinyi Sadallah

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), wamesema wameanza kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali wakilazimishwa wapitishe muswada wa mafao ya viongozi wa kisiasa unaopendekeza wajane na watoto wa marais wastaafu kuanza kulipwa pesheni kila mwezi.

Muswada huo umependekeza wajane na watoto hao kuanza kunufaika na pensheni kila mwezi pale viongozi hao wa kitaifa wanapofariki dunia na kuacha wake na watoto.


Tuhuma hizo wamezitoa wakati wakichagia muswada wa sheria mpya ya maslahi na mafao ya viongozi wa kisiasa ambao umewasilishwa Barazani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk. Mwinyihaji Makame Januari 18 Mwaka huu huko Chukwani mjini Zanzibar.

Wamesema kwamba tangu Wajumbe wa CCM na CUF kuungana wakipinga muswada huo, kumejitokeza baadhi ya viongozi wa SMZ ambao wamekuwa wakitoa vitisho dhidi yao kuwa Baraza hilo litavunjwa iwapo muswada huo utakwama kupitishwa na wao kupoteza kazi.

Akichagia muswada huo mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadhi Salmin, alisema kuna viongozi wamekuwa wakitisha wajumbe kwa kuwaeleza Baraza hilo litavunjwa na kuwataka kubadilisha msimamo wa kupinga muswada huo.

Hata hivyo, hakuwataja vigogo hao wa SMZ lakini alisema hakuna kiongozi mwenye ubavu wa kulivunja baraza hilo iwapo watakataa kupitisha muswada huo kwa kuzingatia maslahi ya taifa na wananchi wao.

Alisemas kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 88, kazi ya Wajumbe katika Baraza hilo ni kutunga sheria na kujadili shughuli za kila Wizara wakati wa kupitia baraza hilo la kutunga sheria Zanzibar.

“Kuna viongozi wanatisha Wajumbe wapya eti Baraza litavunjwa nani mweye ubavu wa kuvunja Baraza tunafanyakzi kutokana na mamlaka tuliyopewa kikatiba kupitia ibara ya 88 ya katiba ya Zanzibar,” alisema Awadhi ambaye pia ni mjumbe wa kamati Kuu ya CCM.

Mwakilishi huo aliwataka wajumbe wa baraza hilo kutekeleza majukumu yao bila ya wasiwasi kutokana na katiba kuwa inawalinda katika kusimamia na kutetea maslahi ya taifa na wananchi wao.

Alisema kwamba ni jambo la kushangaza wananchi wa Zanzibar wanakabiliwa na kero mbalimbali za huduma za jamii ikiwemo tatizo la ukusefu wa maji safi na salama, wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo na kuzorota kwa huduma za matibabu kwa wananchi wa Zanzibar badala yake serikali inapendekeza sheria ya kuwalipa watoto wa marais wastaafu ambao hawajaolewa pamoja na wajane.

Upande wake, Mwakilishi wa (Viti maalum) Asha Bakari Makame, ambaye pia makamu Mwenyekiti wa UWT, alisema serikali ilipaswa kufikiria kuimarisha miundombinu katika maeneo yaliyotegwa kwa miradi ya uwekezaji vitega uchumi huko Fumba kisiwani Unguja na Micheweni Pemba, badala ya kufikiria kutumia mamilioni ya fedha kulipa wajane na watoto wa viongozi wastaafu wa Zanzibar.

Alisema maeneo hayo ya uwekezaji yana umuhimu mkubwa katika kuondoa tatizo la umasikini na kuinua uchumi wa Zanzibar, lakini maeneo hayo yameshindwa kuendelezwa kutokan na tatizo la ukosefu wa miundombinu ya maji, umeme na barabara.

Awali akiwasilisha muswada huo Waziri Dk. Makame alisema muswada huo utawanufaisha viongozi wa kisiasa ambao ni Marais wastaafu, Spika Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Washauri wa Rais Zanzibar.

Hatma ya muswada huo itajulikana leo ambapo Waziri Makame atafunga mjadala na kutoa nafasi kwa wajumbe kupitisha vifungu vya sheria hiyo.

CHANZO : Gazeti la Nipashe

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.