Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuyafanyia kazi malalamiko ya wafanyakazi wa sekta hiyo, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa umakini zaidi.
Maalim Seif ametoa agizo hilo huko hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar baada ya kusikiliza maoni na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo, ikiwa ni kuhitimisha ziara yake aliyoianza wiki iliyopita katika Wizara hiyo.
Amesema aliitisha mkutano huo maksudi kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi, huku akiweka wazi kuwa hawezi kusikiliza maelezo ya viongozi pekee, kwa kuwa wakati mwengine hutoa maelezo ya kujilinda na kujijenga kuliko kuwasilisha mawazo ya wafanyakazi.
Ameitaka Wizara hiyo kuacha tabia ya kutoa majibu ya mkato kwa wafanyakazi kuwa matatizo yao “yatashughulikiwa”, bali ametaka malalamiko yaliyotolewa yawekewe utaratibu wa kuyashughulikia, nay eye apewe ripoti juu ya utekelezaji huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, pia ameonya juu ya kitendo cha kuwahamisha kazi wahariri wawili wa shirika la Utangazaji la Zanzibar upande wa Televisheni kwa visingizio visivyoeleweka.
Wahariri waliohamishwa Televisheni Zanzibar na kupelekwa Idara ya Habari maelezo kwa kisingizio cha kutoa coverage kubwa zaidi kwa Maalim Seif kuliko Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein ni aliyekuwa Mhariri Mkuu wa Shirika hilo Bw. Juma Mohd na msaidizi wake Bw. Ramadhan Ali.
“Wanavyodai viongozi wa Idara hiyo na Wizara kuwa wamekiuka muongozo, lakini nimewambia waniletee huo muongozo hawajaleta hadi sasa. Hivyo inaelekea kuwa hawa wameonewa tu na hatuwezi kukubali kwenda namna hiyo”, alionya na kuongeza;
“Lazima tubadilishe utamaduni wa kuoneana katika serikali, huwezi kumuadhibu mtu kwa kuwa humpendi, mpe vitendea kazi na umuwezeshe, halafu hapo akishindwa mchukulie hatua, lakini sio kwa kuoneana kama hivi. Tena nasema hili halijaishia hapa, nitalifuatilia mpaka nilitie mwisho na nijue ukweli wake”, alifafanua Maalim Seif Seif.
Jumla ya wafanyakazi 12 kutoka Idara mbali mbali za Wizara hiyo walipata fursa ya kutoa maoni yao ambapo wengi walielezea kufarajika kwao na uamuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais kusikiliza maoni ya wafanyakazi.
Wengi kati ya waliopata fursa hiyo walielezea juu ya mazingira magumu ya kazi yenye upungufu wa vitendea kazi vikiwemo usafiri pamoja na ufinyu wa maeneo ya kufanyia kazi.
Sambamba na hilo, wafanyakazi hao walilalamikia maslahi duni wanayopata kutokana na kazi ngumu wanazofanya huku wakikosa malipo ya muda wa ziada pamoja na pesa za likizo.
Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji upande wa Televisheni wamesema wanafanya kazi hadi saa 8 usiku na wakati mwengine hushindwa kurejea majumbani kwao kutokana na tatizo la usafiri na kulazimika kulala kituoni hapo, huku wale wa upande wa Redio wakikabiliwa na tatizo hilo la usafiri na kupelekea kufunguliwa kwa matangazo ya asubuhi kwa wakati.
Bw. Mohd Mustafa Mohd kutoka kamisheni ya Utalii, amesema wakati serikali inajiandaa kuingia katika mpango wa “Utalii kwa wote” ni vyema kituo kikuu cha habari kwa watalii kikafufuliwa ili kutoa taarifa sahihi kwa watalii.
Kabla ya kukutana na wafanyakazi hao Maalim Seif alifanya ziara ya kutembelea Kamisheni ya Utalii na taasisi zake na kuonesha kusikitishwa na mmomonyoko wa fukwe katika chuo cha maendeleo ya Utalii Maruhubi.
Ameitaka Wizara hiyo kulishughulikia kwa haraka tatizo hilo ili kunusuru athari kubwa zinazoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment