Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Ujenzi, nishati ,Ardhi na Makazi Zanzibar Mwalimu Ali Mwalimu, amesema kuwa tatizo kubwa la upatikanaji wa maji mijini na vijijini linatokana na uharibifu wa mazingira katika vianzio vya maji na wananchi kutofuata maelekezo ya kitalamu katika maeneo yao wanayoishi.
Hayo ameyasema leo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Ali Juma Shamuhuna huko Koani Wilaya ya Kati Unguja wakati wa uzinduzi wa kituo cha kulipia huduma ya maji katika sherehe za wiki ya maji duniani ambapo kilele chake kitakua Machi 22 mwaka huu.
Amesema licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya jitihada za makusudi kutatua tatizo la maji linalowakabili wananchi wake bado tatizo hilo linaendelea kuwepo katika maeneo mbali mbali kutokana na baadhi ya wananchi kutofuata maelekezo ya kitaalamu na kusababisha uharibifu wa miundo mbinu jambo linalopelekea upungufu katika visima vya kuzalishia maji
“Tunapoingia katika mikataba na wataalamu wa uchimbaji wa visima hutuuliza hivi sasa mnatumia maji ya kiasi gani na mnahitaji maji ya kiasi gaini,huwajibu kwa ile idadi tunayo taka,visima huchimbwa na hutoa maji mengi tu lakini hatimae maji hayo hupotea”alisema mwalimu.
Amesema hali hiyo imepelekea ukatwaji wa miti ovyo na kusababisha ukame katika maeneo mengi jambo ambalo pia huchochea ardhi kushindwa kutunza maji vizuri katika hali yake ya kawaida
Amesema hali hiyo haiwezi kuvumiliwa hivyo wananchi wanapaswa kubadilika ili waweze kuvitunza vyazio vya maji viweze kuzalisha maji yanayokidhi matumizi yao binafsi na vizazi vinavyokuja.
Amebainisha kuwa Benki ya Dunia imefadhili miradi mikubwa ya maji Unguja na Pemba na kuwataka Wananchi kuendelea kuiunga Mkono miradi hiyo kwa kufuata maelekezo ya wataalamu juu ya kuienzi na kuthamini miradi hiyo.
“kuna watu wamejenga mahodhi makubwa kwa kuhifadhia maji kwa wingi yao na wezao ,lakini kikawaida wajue hodhi lazima livuje hata ufanye vipi,hii sitabia nzuri kwani nayo huchangia wananchi wengine kukosa huduma ya maji ”aliongezea Mwalimu.
Ili kufanikisha huduma hiyo Mwalimu aliwataka wananchi kuendelea kulipa kodi ya maji kwa kiasi cha Shilingi 2,000 kwa mwezi kwani kufanya hivyo pesa hizo husaidia Shirika kuweza kujikimu kununulia vifaa na matengenezo pale tatizo linapojitokeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mustafa Makame Ibrahim aliwataka wananchi wa mkoa wake kukitumia kituo hicho kwa kulipia maji na kutoa taarifa mbali mbali zinazo husiana na uharibifu wa miundo mbinu ya maji na kupatiwa ufumbuzi.
Kituo hicho awali kilikua jengo la Mkuu wa Mkoa ambacho kimegharimu shilingi milioni nne na laki tano kwa fanicha za kiofisi na pia kitatumika kwa shughuli za mahakama ya ardhi.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO
No comments:
Post a Comment