Habari za Punde

Zanzibar Mwenyeji wa Mkutano Mkuu Klabu za Mashirika ya Ndege Duniani

Na Abdi Shamnah

ZANZIBAR imeteuliwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 45 wa Klabu za Mashirika ya Ndege Duniani (WACA), unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Oktoba 7, mwaka huu.

Mkutano huo wa mwaka, utafanyika katika Hoteli ya Sea Cliff, ilioko Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, kuanzia Oktoba 7 hadi 12, 2012 na kuwashirikisha washiriki wapatao 200 kutoka klabu za Mashirika ya ndege Duniani.


Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, WACA imefikia uamuzi wa kuiteua Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huo, kutokana na juhudi zilizofanywa Kamisheni hiyo katika mikutano na matamasha mbali mbali nje ya nchi, katika kuhakikisha Zanzibar inaunganishwa na Dunia katika nyanja za safari za anga .

Lengo la mkutano huo ni kuwakusanya pamoja wamiliki wa mashirika ya ndege wanaounda Jumuiya hiyo kwa dhamira ya kuongeza ustawi katika mazingira ya safari za anga na kukuza mafahamiano miongoni mwa mashirika hayo, ili kuona utalii unachukua nafasi yake kikamilifu.

Katika taarifa Yake Kamisheni, imeelezwa kuwa kufanyika kwa mkutano huo kutatoa fursa kwa mashirika mbali mbali ya Ndege Duniani ,kuvutika na kufanya safari zake hapa nchini.

Hii ni mara ya kwanza kwa WACA kuandaa mkutano na kukusanya na washirki wengi zaidi duniani, ambapo Zanzibar mbali na kutokuwa na Shirika la ndege, itaweza kunufaika sana katika azma yake ya kukuza soko la Utalii kutoka pande zote za Dunia.

‘Mkakati wetu mkubwa la kukuza soko la utalii, na hiyo itafikiwa kwa kuwepo mashirika mengi zaidi ya ndege yatakayovutika na kufanya safari zake nchini, hatua itakayoongeza idadi ya ujio wa watalii katika visiwa vyetu’, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kamisheni imefarijika mno, Zanzibar kupata fursa hiyo adhimu, na tayari inajipanga kuhakikisha washiriki na wageni wote watakaohudhuria mkutano huo wanafurahia kuwepo kwao Zanzibar, ikizingatia kuwepo Hoteli kubwa nzuri na vyumba vya kutosha vya kulaza wageni mashuhuri.

Aidha katika hatua ya kuupa heshima na kuutangaza vilivyo mkutano huo kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo anatarajiwa kuwa mwenye ngazi ya Waziri kwenda juu.

Tayari WACA imeandaa mikutano kama hiyo katika nchi mbali mbali Duniani, zikiwemo nchi za Kenya na Afrika Kusini kwa upande wa Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.