Mwajuma Mmanga na Kauthar Abdalla
IDARA ya Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto imesema wakati umefika kufanyiwa mapitio na marekebisho juu ya vikwazo vya kisheria dhidi ya ushahidi kwa watoto walemavu wanaofanyiwa udhalilishaji.
Akizungumza na Gazeti hili huko ofisini kwake Vuga mjini hapa, Mkurugenzi wa Idara hiyo Rahma Ali Khamis, alisema kesi nyingi za udhalilishaji hasa kwa watoto na wanawake, washitakiwa hushindwa kutiwa hatiani kutokana na vikwazo mbali mbali vya kiushahidi.
Alisema mazingira ya ushahidi yanayozungumzwa hivi sasa katika sheria hayaendani na wakati uliopo jambo ambalo linazifanya kesi za aina hiyo washitakiwa washindwe kutiwa hatiani.
Mkurugenzi huyo alisema idara hiyo itavifanyia mapitio vikwazo vya kiushahidi dhidi ya kesi hizo ili wanapofikishwa mahakamani sheria iweze kuwatia mikononi.
Akizungumzia unyanyasaji wa watoto wenye ulemavu, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi hizo ambapo katika wilaya nne za Unguja wapo watoto wenye ulemavu 2853.
Aidha alisema kuwa haki ya watoto wenye ulemavu ni jukumu la kila mtu ili kuhakikisha kila mmoja anazilinda, anaziheshimu, anaziendeleza pamoja na kuzitimiza tokea katika ngazi za familia.
Katika kuhakikisha kwamba mtoto anapata haki zake za msingi na kuondokana na unyanyasaji nchi wanachama za Afrika zote zinaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kila ifikapo Juni 16, ya kila mwaka.
Alifahamisha kuwa chanzo cha kuadhimishwa siku hiyo ni maamuzi kutoka kwa kamati ya ustawi wa Afrika ili kuwakumbuka watoto wa Suweto ambapo mamia ya watoto walipoteza maisha yao kwa kuuliwa na maaskari wa makaburu mwaka 1976,kutokana na kudai haki yao ya kutumia lugha hiyo.
“Mamia ya watoto wa Afrika walipoteza maisha yao kutokana askari kuwauwa mnamo mwaka 1976, kutokana na kudai haki yao ya kutumia lugha waitakayo ambapo kamati ya ustawi wa Afrika imeamua kufanya maadhimisho ya siku ya mtoto kwa lengo la kuwakumbuka”, alisema Mkurugenzi.
Pia alisema kusainiwa kwa mkataba mwaka 2003 na Tanzania uliozungumzia haki zote za mtoto wa Afrika ndio chanzo kikuu cha kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
Hata hivyo alielezea kuwa sera ya haki ya mtoto haikumbagua mtoto mwenye ulemavu pekee bali hakuna mtu yoyote mwenye haki ya kumnyanyasa wa aina yoyote.
Rahma alisema bado jamii haijaweza kufikia vilivyo katika kuelimisha na kutoa taaluma juu ya umuhimu wa kumtunza mtoto na kumpa haki zake.
Aliiomba jamii kujali watoto kama ni matunda yao wenyewe kwani hali kubwa ya jamii inatelekeza watoto baada ya ndoa kuvunjika.
Pamoja na hayo aliziomba nchi wanachama zote za afrika ambazo ni 63, kuchukuwa hatua za makusudi ili watoto wapate haki zao.
No comments:
Post a Comment