Habari za Punde

Wawakilishi : siasa zisitugawe utoaji maoni

Na Ramadhan Makame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamesema wananchi wa Zanzibar, wasigawanyike kwa misingi ya kisiasa na misimamo ya vyama vyao katika wakati huu ambapo maoni ya katiba mpya ya Tanzania yanakusanywa.

Wakichangia hotuba ya bajati ya wizara ya Katiba na Sheria, wakilishi hao walisema Wazanzibari waakuwa wamefanya kosa kubwa endapo watakubali kuwanyika katika kutoa maoni kwa misingi ya utashi wa vyama vyao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, alisema huu ni wakati muhimu kwa Wazanzibari kuunganisha nguvu na kuwa na ajenda moja katika kutoa maoni yao.

Alisema wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana hazikuunga kwa misingi ya vyama, na kupendekeza kuwa vyama vya siasa ama itikadi zao walizonazo hivi sasa zisitumike kuwagawa katika utoaji wa maoni ya katiba mpya.

Naye Mwakilishi wa jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk, alisema wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni yao ili kujadili mustakbali wa nchi yao na kueleza kuwa waeleze lile wasilolipenda.

Kwa upande wake akiwasilisha hotuba ya wizara hiyo, waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, aliwataka wananchi wanaotoa maoni juu ya katiba mpya, kuhakikisha maoni yao yanalenga kuinua maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi na mapato ya wizara yake.

Alisema jambo la muhimu ni kuhakikisha maoni yanayotolewa na wananchi yalenge maslahi ya Zanzibar na kuiwezesha kuwa na haki na uhuru kamili ndani ya Muungano.

Alisema kutekelezwa hayo kutaiwezesha Zanzibar kutekeleza mambo yake ya kimaendeleo bila ya kuingiliwa na kueleza kuwa wizara yake itasimamia yote ambayo wananchi watayapendekeza.

“Lengo letu ni kuifanya Zanzibar kuwa na haki na uhuru wake kamili ndani ya Muungano wetu, lengo ambalo litaifanya Zanzibar kutekeleza mambo yake ya kimaendeleo bila ya kuingiliwa”,alisema waziri huyo.

Akizungumzia Idara ya Mahakama, waziri huyo alisema upo mrundikano wa kesi nyingi zilizokuwa hazijatolewa maamuzi, ambapo kutokamilishwa kwa uchunguzi ndicho kikwazo kikubwa cha kushindwa kutolewa maamuzi.

Alisema kati ya mwezi Julai hadi Machi mwaka 2012 jumla ya kesi 5,477 zilifunguliwa katika mahakama za Zanzibar zikiwemo za jinai na madai lakini ni kesi 2,604 ambazo ni sawa na asilimia 48 ndizo zilizotolewa maamuzi.

“Picha hii inaonesha kuwa bado kuna kesai nyingi ambazo hazijatolewa uamuzi na hivyo kuna mrundikano wa kesi”,alisema waziri huyo.

Waziri huyo alisema wizara hiyo inakerwa sana na baadhi ya wafanyakazi wakiwemo makarani na mahakimu kujihusisha na rushwa hasa kwenye kesi za dawa za kulevya, ubakaji na mashauri yanayohusu migogoro ya ardhi.

“Haya ni miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa sana na wananchi, Mheshimiwa Spika, hata mimi yananikera sana na hivi sasa tumeshaanza kuyachukulia hatua”,alisema waziri huyo.

Abubakar aliwatanabahisha wananchi kuwa kuwa mali za wakfu ni mali za waumini na sio za serikali na kwamba wapangaji waache kuzikodisha mara nne au tano ya zaidi ya waliokodishwa wao na kutochukua vilemba.

“Kuchukua vilemba ni sawa na kuwaibia au kuwanyang’anya wanufaika wa wakafu Mwenyezi Mungu hayuko radhi nao kwa hilo na sisi tulipewa dhamana tukibaini hilo tutachukua haua kali kwa mujibu wa sheria”,alisema waziri huyo.

Waziri huyo aliliomba Baraza limuidhinishie shilingi bilioni 7,591,000,000 kwa mwaka 2012/2013, fedha ambazo zitatumika kwa matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Akichangia hotuba hiyo kwa niaba ya kamati ya Katiba Sheria na Utawala, Wanu Hafidh Ameir, elimu ya katiba mpya ilipaswa kutolewa kabla ya zoezi la kukusanywa maoni.

Alitaka wizara hiyo kuhakikisha inawashughulikia mahakami na majaji wanaolalamikiwa na wanachi juu ya kujihusisha na vitendo vya ulaji rushwa.

Akichangia hotuba hiyo, Mwakilishi wa jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk alisema kipato kidogo cha mshahara kwa makarani wa mahakamani ndicho kichocheo cha vitendo vya rushwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.