Habari za Punde

Maalim Seif ahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha vitambulisho vya Taifa

 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akifungua tawi la Chama hicho katika jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.
 Mbunge wa jimbo la Magogoni Hamadi Ali Hamadi (CUF) akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi la CUF katika jimbo hilo pamoja na utoaji wa baiskeli wa watendai wa matawi. Hafla hiyo ilihududhuriwa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi la Chama hicho jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja
 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi la Chama hicho jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi baiskeli tisa kwa makatibu wa matawi ya CUF jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa linalotarajiwa kuanza hivi karibuni hapa Zanzibar.
 
Amesema suala la vitambulisho limekuwa na umuhimu wa kipekee duniani katika kutunza kumbukumbu na mipango ya kitaifa, hivyo wananchi wasipuuze kujiandikisha kwa ajili ya vitambulisho hivyo.


“Wananchi tafadhalini musipuuze, nendeni mukajiandikishe ili mupate vitambulisho vya Taifa, na nakwambieni mukija mukipuuza mutakuja juta baadae”, alitahadharisha Maalim Seif na kuongeza,
“Hivi sasa tunasikia kuna baadhi ya maeneo wananchi waliokataa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makaazi iliyomalizika hivi karibuni nchini kote, hawapatiwi huduma katika maeneo yao, kwa hivyo nakunasihini sana wananchi musipuuze kabisa”, alisisitiza.
 
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa CUF na wananchi baada ya kufungua tawi la Chama hicho katika jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.
 
Aidha Maalim Seif aliwaonya watendaji wanaoendelea kuwahangaisha wananchi wakati wanapoomba kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi kuwa, kuwa wanakwenda kinyume na maagizo ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein, na kwamba watachukuliwa na hatua za kisheria kwa kukaidi amri hiyo.
 
Amesema katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Pemba pamoja na Mkoa wa Kaskazini Unguja, hali ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo imekuwa ikienda vizuri lakini tatizo kubwa zaidi limekuwa likijitokeza katika Mkoa wa Mjini Magharibi, jambo ambalo halitofumbiwa macho.
 
“Vitambulisho hivi ni haki ya kikatiba ya kila Mzanzibari aliyetimiza masharti ya ukaazi, leo anajitokeza sheha anawaambia wananchi kuwa hatoi barua hadi mtu atimize umri wa miaka 50”, alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF huku akitaka kupatiwa jina la sheha huyo.
 
Amewataka watendaji wa ofisi ya vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka kutumiwa vibaya na viongozi kwa maslahi ya kisiasa.
 
“Unapomkosesha mwananchi kitambulisho unakusudia nini, huu ni ukiukwaji wa katiba na lazima tuukomeshe”, aliongeza.
 
Akizungumzia kuhusu nia ya kujiuzulu kwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Ismail Jussa Ladhu, Maalim Seif amewathibitishia wanachama juu ya ukweli wa jambo hilo, na kuwataka wasifadhaike kwani anafanya hivyo kwa nia njema.
 
“Jussa bado ni mwanachama kindakindaki wa CUF na ni mjumbe wa baraza kuu la uongozi ndani ya Chama chetu, lakini baada ya kutuletea maoni yake nikiwa mimi, Profesa Lipumba na Makamu Mwenyekiti Mhe. Machano Khamis, tuliona sababu zake ni za msingi na hakuna haja ya kumzuia kutimiza maamuzi yake”, alisema.
 
Amesema ifikapo tarehe 10 mwezi huu, Jussa atakuwa si Naibu Katibu Mkuu tena wa Chama hicho, na kwamba viongozi wanatafakari juu ya kumpata mwanachama atakae kaimu nafasi hiyo.
 
Ametaja sababu za msingi zilizotolewa na Jussa kutaka kujiuzulu kuwa ni pamoja na kumuwezesha kupata muda wa kutosha kushugulikia maendeleo ya jimbo lake la Mji Mkongwe pamoja na kufanya utafiti kabla ya kuibana serikali katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.
 
Katika Mkutano huo, Maalim Seif alikabidhi baiskeli tisa kwa ajili ya makatibu wa matawi ya CUF katika Jimbo la Magogoni, kigari kwa ajili ya bwana Ali Khamis Ali (mwenye ulemavu), pamoja na shilingi laki tatu kwa ajili ya kikundi cha ushirika cha Jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.