Na Hafsa Golo
KAMPUNI ya Bopar Enterprises Limeted ambayo ndiyo
iliyoingiza unga mbovu kupitia bandari ya Zanzibar
imesema itatekeleza agizo la serikali la
kuuondoa unga huo.
Wiki iliyopita, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Maalim Seif Sharif Hamad alitoa mwezi mmoja kwa kampuni hiyo kuundoa unga huo
ambao tayari umeanza kutoa harufu mbaya.
Hata hivyo kampuni hiyo imetaka kampuni ya uwakala wa
mizigo bandarini kutoa mchango wake ili unga huo uondoke katika bandari hiyo
kwa kuwa ndiyo iliyozembea hadi kusababisha unga huo uharibike.
Meneja wa kampuni hiyo, Said Nassir Nassor amesema kama
kampuni hiyo ya uwakala wa mizigo itakataa kutoka ushirikiano, kampuni yake
itauondoa unga huo na baadae kuchukua hatua nyengine za kisheria.
Alisema hakuna
sababu ya kupinga amri ya serikali kwani kampuni yake inaheshimu maamuzi hayo
hasa ikizingatia kwamba serikali ndio
muhimili mkuu katika nchi.
Meneja huyo alisema unga huo ulinunuliwa ukiwa bado
haujaharibika, lakini ulikaa muda mrefu baharini na kusababisha kuharibika.
Alisema makontena yenye unga huo yaliondolewa nchini
Uturuki Disemba 4, 2011 na kufika bandari ya Dar es Salaam Januari 3, 2012
lakini ulifikishwa bandari ya Zanzibar
mwezi Mei mwaka 2012.
"Joto na hali ya hewa ya bahari lazima unga uharibike
miezi minne unga upo baharini mimi nawalaumu wenye meli na hili mlibaini kwani
unga wa ngano hauwezi kustahamili na kawaida unaishi kwa muda wa miezi tisa
zaidi ya hapo unaharibika,"alisema.
Gazeti hili ilipata ‘bill of lading’ yenye namba MSCUOS
001680 ambayo imeainisha tarehe
uliotoka unga huo nchini Uturuki.
Meneja wa kampuni ya Mediterranean shiping tawi la Zanzibar,
Abdurazak Omar Tahir, alisema wao hawahusiki
na uondoshaji wa makontena ya unga huo kwani sio kazi yao.
Aidha alisema kutokana na dalili zilizojitokeza unga huo ulipakiwa tayari ukiwa umeanza kuharibika na
kutokana na masafa marefu ya usafiri na kuchelewa kwa taratibu za ufungaji gati na upakuaji katika wa bandari ya Dar -es Salaam
, unga huo ulizidi kuharibika.
No comments:
Post a Comment