Na Mwantanga Ame
MKE wa Rais wa Zanzibar, mama Mwanamwema Shein, amewataka wanawake wa UWT Mkoa wa Mjini Magharibi, kuvifanya VICOBA na SACCOSS kuwa na uwezo wa kukopesheka benki, badala ya kuwaza kutumia fedha zao kununulia nguo za madira.
Mama Shein, aliyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya VICOBA kwa wanawake wa UWT, yanayofanyika kwa siku tatu katika ofisi ya CCM Mkoa wa Mjini, Amani Zanzibar.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, mama Asha Suleiman Iddi, aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoisoma kwa niaba ya mama Shein.
Alisema ni vyema wanawake wa mkoa huo wakaacha tabia ya kupenda kununua nguo na badala yake watumie fedha zao kukuza SACCOS zao, ili ziweze kukopesheka benki.
Alisema wanawake wameanza kujiunga katika vikundi vya SACCOSS na VICOBA, lakini vinaweza visiwanufaishe ikiwa watashindwa kujipanga kukuza mitaji yao.
Alisema, SACCOSs na VICOBA, dhamira ya kuwaokowa wanawake wa Tanzania na lazima wanaojitolea kujiunga nazo wahakikishe mitaji inakua.
Alisema serikali ina matumaini makubwa kuanza kwa huduma ya VICOBA ndani ya Jumuiya ya UWT kwa kiasi kikubwa kutainua hali za wanachama wa umoja huo.
Aliwataka wanachama wa taasisi hiyo, kuzingatia umuhimu wa kushiriki katika vikao vya mfuko huo, kwani haitakuwa busara kutumia nafasi zao kulalamika nje ya vikao.
Pia aliwaasa wanawake hao kutokubali kutumiwa wakati wa kutafuta uongozi kwani baadhi ya watu wameamua kuliandama kundi hilo kwa maslahi binafsi.
Katika uzinduzi huo, mama Shein alikabidhi shilingi milioni 2,000,000 ikiwa ni mchango wa pamoja na wake wa viongozi wa umoja anaousimamia huku mama Asha na mumewe walichangia shilingi milioni 1,000,000 na Mbunge wa wanawake, Faharia Shomari alichangia milioni 10.
Michango mingine ilitolewa na wanachama baada ya kuendesha harambee ya kuchangia mtaji wa mfuko huo ambapo fedha hizo zilifikia shilingi milioni 13.405.
Naye Msimamizi wa mafunzo hayo, Mgeni Hassan Juma, aliwataka wanachama wa Jumuiya hiyo, kufuatilia kwa vitendo mafunzo hayo ili yaweze kuwanufaisha.
Mbunge wa wanawake, Faharia Shomari, aliwataka wanawake wa mkoa huo kuendelea kushikamana ili kuimarisha chama na umoja huo.
Akitoa shukrani Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini, Fatma Shomari, alisema kuja kwa mfuko huo kutaongeza vipato vya wanawake.
No comments:
Post a Comment