Habari za Punde

Sekta ya Utalii Inakabiliwa na Changamoto Nyingi -- Waziri.

Na Asya Hassan
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, imesema sekta ya utalii bado inakabiliwa na changamoto kubwa ambayo inapelekea kukwamisha juhudi zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha utalii unakuwa na kupata wageni wenye hadhi ya daraja la juu.

Imesema kutokana na hali hiyo ni vyema kwa kamati za utalii za Wilaya na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kutambua kwamba wana jukumu kubwa la kubuni mikakati na njia imara na endelevu ambazo zitasaidia kutatua changamoto hizo.

Waziri wa Wizara hiyo Said Ali Mbarouk alieleza hayo katika semina ya Kamati za Utalii za Wilaya iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Alisema kamati hizo ni vyema kubuni vivutio vipya vya utalii ambavyo vitaweza kuongeza kasi katika kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kuwa utalii ni biashara inayobadilika kila kukicha ambapo katika siku za hivi karibuni mabadiliko yamekuwa makubwa kutokana na mwendo kasi wa sayansi na teknolojia.

"Naamini kutokana na hali hiyo akili ya ubunifu pekee ndio itakayoweza kukabiliana na mabadiliko hayo,"alisema Waziri huyo.

Waziri huyo akiitaja changamoto nyengine alisema kuwa ni ile ya kutegemea soko la nchi za Ulaya Kusini (Italy,England,Spain,Germany) na kwa kiasi fulani Marekani (USA), Nchi hizo katika miaka ya hivi karibuni hali zao za kiuchumi zimekuwa siyo nzuri hivyo idadi ya watalii wanaotoka katika nchi hizo imepungua.

Hata hivyo alifahamisha kuwa ili kuweza kukabiliana na hali hiyo hakunabudi kuanza sasa kusaka masoko mapya katika nchi za Ulaya Mashariki,China,Mashariki ya mbali ,Uarabuni na Afrika huku yakiimarishwa masoko ya asili ili kuweza kupata kuboresha sekta hiyo.

Aidha alifahamisha kuwa ipo haja ya kuweza kukabiliana na baadhi ya wadau wa utalii ambao wanafanya shughuli zao bila ya kuzingatia sheria za nchi na zile za utalii.

Waziri Mbarouk alifahamisha kuwa sekta ya utalii ina jukumu kubwa katika ukuzaji wa uchumi wa Zanzibar na hatimaye kufikia lengo la kupunguza umaskini wa wananchi wake.

Sambamba na hayo Waziri huyo alifahamisha kuwa dira ya 2020 na mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA) kwa pamoja vinalenga kufikia ukuwaji wa uchumi utakaowajali hasa walio maskini.

Alifahamisha kuwa toka kuanza kupewa kipaumbele kwa sekta hiyo katika kipindi cha miaka ya 80, baada ya mageuzi ya kiuchumi yaliofanyika hapa Zanzibar yaliotokana na kuporomoka kwa zao la karafuu ambapo hali hiyo iliweza kuleta mabadiliko yenye mafanikio katika uchumi.

Akizitaja takwimu Waziri huyo alifahamisha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita sekta hiyo inaonesha kuwa imepata mafanikio makubwa ikiwemo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchi na kufikia watalii 169,229 kwa mwaka 2012.

Alisema kuwa sekta hiyo ina faida kwani kwa kupitia mahoteli yenye hadhi ya juu imeweza kuongeza miundombinu ya barabara,bandari na uwanja wa ndege imeimarika pamoja na wigo wa masoko nao pia umekuwa kwa kiasi kikubwa.

Alifahamisha kuwa ni tegemeo la serikali kuwa kamati za utalii za Wilaya zitasaidia kutoa mwelekeo juu ya kuweza kuuendeleza utalii ambao utalinda mila silka na utamaduni wa mzanzibar na wakati huo huo kuweza kuvutia wageni wenye hadhi.

"Tunafahamu kuwa utalii hapa Zanzibar ndio sekta kiongozi katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwani inachangia wastani wa asilimia 27% ya pato la Taifa na wastani wa asilimia 80% ya fedha za kigeni zinatokana na sekta ya utalii,"alisema.

Alifahamisha kuwa utalii kwa ujumla wake unasaidia na unaendelea kusaidia kwa kutoa ajira kwa wazanzibar mbalimbali ambapo kiasi cha watu 13,000 wamepata ajira ya moja kwa moja na wengine wapatao 46,000 wanategemea kipato chao kupitia sekta hiyo kwa kuuza au kutoa huduma mbalimbali.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, alisema msingi mkubwa wa semina hiyo ni kuwaelimisha na kuwafahamisha viongozi wa kamati hizo ili kuweza kutekeleza kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wa mtoa mada ya utalii Zanzibar, Said Soud, alisema sekta ya utalii inasaidia kwa kiasi kikubwa Zanzibar kwani kuwepo kwa sekta hiyo inasaidia kukuwa kwa uchumi,kijamii na miundombinu nchini kuzidi mwaka hadi mwaka kwa asilimia 6.5% pamoja na kuongezeka uwekezaji ambapo asilimia 72% hivi sasa ya wawekezaji wamejikita katika utalii.

Kwa upande wa washiriki hao walitaka serikali kuangalia kwa kina suala la ajira katika sekta hiyo kwani bado halijatendewa usawa kwa wageni na wazalendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.