Mkurugenzi Idara ya Diaspora
Z’bar afariki
Marehemu Khamis Ali Khamis
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora
katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Khamis Ali Khamis (pichani),
amefariki dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 52.
Alifariki nyumbani kwake Mkele
usiku wa kuamkia jana baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa shinikizo la damu.
Juzi marehemu alishiriki hafla
ya kumpokea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliekuwa
akitokea Comoro katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Marehemu alianza elimu yake ya
msingi mwaka 1969 na kumalizia elimu ya sekondari mwaka 1983.
Mwaka 1986 alianza masomo ya stashahada
ya lugha katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) na baadae
masomo shahada ya kwanza ya sayansi ya uchumi nchini Yugoslavia mwaka 1986 hadi
mwaka 1993, ambako alifaulu na kutunukiwa shahada.
Mwaka 1996 hadi 1997 alifanya shahada
ya uzamili ya mipango ya maendeleo vijijini nchini India.
Aidha alihudhuria masomo mafupi
ya fani mbali mbali ndani na nje ya nchi kama vile ushirikiano wa kimataifa, sera
kuhusiana na masuala ya uongozi, uchumi na utafiti na nyengine nyingi.
Alianza utumishi wa umma mwaka
1985 alipoajiriwa na Wizara ya Biashara, Viwanda na Utalii katika hoteli ya Bwawani
akiwa mpokezi wa wageni.
Mwaka 1993 hadi 1994 alikuwa Ofisa
wa Mapato katika Kamisheni ya Utalii ambapo baadae mwaka huo aliteuliwa kuwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mipango katika Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uchumi Zanzibar.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa
msaidizi mwandishi wa hotuba za Rais katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Zanzibar, 2008 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Mawasiliano na Habari Ikulu Zanzibar.
Mwaka 2011 aliteuliwa Mkurugenzi wa Idara ya
Uratibu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Wazanzibari Waliopo Nje (Diaspora)
wadhifa ambao aliendelea nao hadi kufariki kwake.
Katika kipindi chote cha
utumishi wake, marehemu alikuwa mchapa kazi hodari na mwenye kufanya kazi kwa ushirikiano
na wenzake.
Marehemu ameacha vizuka wawili
na watoto wanne, Mwenyezi Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu, Amiin.
No comments:
Post a Comment