Habari za Punde

Historia kuanzisha Vyuo Vikuu Zanzibar na Comoro Zinafanana.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                           19 Septemba, 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema historia ya kuanzishwa vyuo vikuu Zanzibar na Muungano wa Comoro inafafana.
Amesema hadi miaka 18 iliyopita Zanzibar haikuwa na chuo kikuu na vijana wa Zanzibar walilazimika kupata elimu ya chuo kikuu Tanzania bara ama nje ya nchi kama walivyolazimika vijana wa Comoro hadi miaka michache iliyopita.
Dk. Shein alisema hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Kitivo cha Dini ya Kiislamu na Lugha ya Kiarabu cha Chuo Kikuu cha Comoro, Dk. Said Bourhani Abdallah, alipotembelea chuo hicho hivi karibuni wakati wa ziara yake nchini humo iliyomalizika jana.
Alimueleza Dk. Said ambaye aliambatana na uongozi mzima wa kitivo hicho kuwa historia hiyo inatokana na kutawaliwa hivyo wakati huu wa kujitawala taasisi za elimu ya juu za Comoro na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zina wajibu wa kushirikiana na kusaidiana ili kuwapatia watu wake maarifa ya kuendeleza nchi zao.
Alifafanua kuwa Zanzibar ilianza na chuo kikuu binafsi na baadae kuanzishwa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA ambapo sasa Zanzibar ina vyuo vikuu vitatu ikiwa ni miongoni mwa idadi ya vyuo vikuu zaidi ya 30 vilivyoko Tanzania.
Aliongeza kuwa chuo kikuu cha serikali SUZA ambacho hakikuanzishwa muda mrefu lakini kimekuwa kikipanuka kwa haraka sana hivyo kuwa na uwezo wa kufundisha masomo na fani mbalimbali za elimu.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa, kwa mujibu wa mfumo wa uongozi wa elimu nchini, elimu ya juu ni suala la muungano hivyo linasimamiwa na taasisi maalum za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa hivyo alizidi kubainisha kuwa taasisi hizo husimamia vyuo vikuu tangu kuanzishwa hadi kuangalia ubora wa elimu itolewayo ambapo kwa utaratibu huo vyeti na shahada mbalimbali zitolewazo na vyuo hivyo vinatambuliwa ulimwenguni kote.
Dk. Shein alisema elimu ni moja ya eneo ambalo limechukua nafasi kubwa katika mazungumzo yake na Rais wa Muungano wa Comoro Dk. Dhoinine Ikililou wakati wa zaiara yake nchini humo hivyo inakusudiwa watalaamu wa pande mbili hizo watakutana kujadili kwa undani zaidi namna ya kushirikiana.
Aliongeza kuwa utaratibu utafanywa wa kumuwezesha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar-SUZA kutembelea Chuo Kikuu cha Comoro kuzungumzia suala hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo hicho Dk. Said Abdallah alimueleza Mhe Rais kuwa uanzishwaji wa chuo kikuu nchini Comoro ni changamoto ambayo wamekuwa wakipambana nayo tangu kupata uhuru.
Alieleza kuwa jitihada za marais mbalimbali walioongoza nchi hiyo zilifanyika kuanzisha chuo kikuu na mwaka 2003 wakati wa uongozi wa Rais Ahmed Abdulla ndipo ilipowezekana lakini katika mazingira magumu.
Dk. Said anasema wananchi wa nchi hiyo wanaamini kuwa ni utashi wa kisiasa ambao umeiwezesha Comoro kupata chuo kikuu chake ambapo sasa vijana wa nchi hiyo hawalazimiki kwenda nje kupata elimu ya juu.
Hata hivyo Dk. Said aliongeza uendeshaji wa chuo hicho hautegemei tu serikali bali uongozi wa chuo umekuwa ukijithidi kutafuta misaada toka washirika wa maendeleo pamoja na kufanya mawasiliano na taasisi za elimu ya juu za ukanda huu zikiwemo za Tanzania.
Alibainisha kuwa Chuo hicho tayari kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na wana matumiani makubwa ushirikiano huo utakuwa wa manufaa kwa pande zote.
Kabla ya mazungumzo hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ujumbe wake ulipata fursa ya kutembelea sehemu mbali mbali za kitivo hicho na kuona majengo ya zamani ya kitivo hicho na majengo mapya ya chuo.  
Dk. Shein alimaliza ziara yake ya siku nne katika Muungano wa Comoro jana asubuhi na kurejea nyumbani baadae nchana.
Katika ziara hiyo alifuatana na mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Naibu wa Waziri wa Kilimo na Maliasili Bibi Mtumwa Kheir Mbarak na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwezeshaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bwana Ali Saleh Mwinyikai, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Ali Abdulla na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Bwana Kombo Abdulhamid Khamis. 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.