STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
13.12.2014

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Wabunge wa Bunge la
Ireland na kuwaeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa huku viongozi hao wakiahidi
nchi yao kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Wabunge hao huko Ikulu mjini
Zanzibar ambapo wabunge hao waliongozwa na Balozi wa Ireland nchini Tanzania
Mhe. Fionula Gilsenan.
Katika maelezo
yake Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao hatua mbali mbali zilizopitiwa katika
kuanzisha Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ikiwa ni pamoja na
marekebisho katika vipengele vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Dk. Shein
alieleza kuwa kuwepo kwa Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa hapa nchini kumeweza
kuleta mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na mashirikiano katika kuendeleza na
kukuza uchumi wa nchi sambamba na kuimarisha amani na utulivu uliopo.
Alisisitiza kwamba
kubwa kuliko yote ni kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo hapa nchini
ambapo yeye akiwa ni kiongozi na Rais wa Zanzibar ameweza kuhakikisha hilo
linaendelezwa kwa mashirikiano ya wananchi na viongozi wao.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa Ireland kwa kuendeleza ushirikiano
na uhusiano kati yake na Zanzibar na kusisitiza haja ya kuimarishwa zaidi ushirikiano
kupitia Shirika lake la misaada.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo imeweza kusaida katika sekta ya afya,
miundombinu na mawasiliano, huduma za zimamoto, ufugaji na sekta nyenginezo.
Dk. Shein pia,
aliueleza uongozi huo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya uvuvi na kueleza changamoto zilizopo
hivi sasa ikiwa ni pamoja na azma ya kufikia uvuvi katika bahari kuu hatua ambayo
inaweza kuungwa mkono na nchi hiyo ambayo tayari imepata mafanikio katika sekta
hiyo.
Alisema kuwa bado
kuna eneo kubwa la bahari ya Zanzibar ambalo halijafikiwa katika kutekeleza
shughuli za uvuvi licha ya kuwa na rasilimali za kutosha, hiyo ni kutokana na
ukosefu wa miundombinu na utaalamu katika kuendeleza sekta hiyo.
Katika maelezo
hayo pia, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao juhudi zinazochukuliwa na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii ambayo ni sekta mama
katika kuinua uchumi wa Zanzibar.
Dk. Shein
aliwataka viongozi hao kuitumia fursa hiyo ya ziara yao hapa Zanzibar kwa
kutembelea katika maeneo mbali mbali ya kitalii ili waweze kuwa mabalozi wazuri
wa kuitangaza Zanzibar nchini kwao.
Nao viongozi hao
kwa nyakati tofauti walieleza kufarajika kwao katika ziara yao hapa Zanzibar
sambamba na mapokezi mazuri waliyoyapata ambayo yanatokana na ukarimu wa
Wazanzibari wa kupenda wageni huku wakipongeza mafanikio ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa chini ya uongozi wa Dk.
Shein.
Wabunge hao
walitumia fursa hiyo kueleza mafanikio
ya kisiasa yaliopatikana nchini Ireland pamoja na changamoto mbali mbali
zilizopo ambazo hivi sasa zimeweza kupatiwa ufumbuzi kwa mashirikiano ya nchi
mbali mbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Canada, Jumuiya ya Ulaya na
nyenginezo.
Aidha, Wabunge
hao mbali ya maelezo yao kadhaa pia, walimueleza Dk. Shein juhudi
wanazozichukua katika kuhakikisha ushirikiano na uhusiano kati ya Ireland na
nchi za Afrika unaendelezwa kupitia Umoja wa Wabunge wa Afrika na Ulaya
‘AWEPA’.
Wabunge hao
kutoka chama tawala na chama cha upinzani nchini Ireland, pia walieleza
mashirikiano yaliopo kati ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania na Bunge la Ireland
ambapo ujio wao unatokana na uhusiano mwema wa pande hizo ambapo tayari Wabunge
wa Tanzania wameshafanya ziara kama hiyo mwezi
Julai mwaka huu kwa lengo la kujifunza na kukuza ushirikiano wa pamoja.
Wakieleza lengo
la uhusiano na ushirikiano huo ni pamoja na kuendeleza maeneo ambayo bado
hayajapewa kipaumbele likiwemo eneo la uvuvi ambalo ukusanyaji wake wa mapato
ni tofauti na sekta nyengine, hivyo linahitaji msukumo.
Miongoni mwa
viongozi walioambatana na Wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Wawi Mhe.
Hamad Rashid Mohammed akiwa pamoja
na maafisa wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment