STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dar-es-Salaam
13.12.2014

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza ushirikiano na maelewano ndani
ya vilabu pamoja na taasisi zinazosimamia michezo nchini na kukipongeza Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa kazi nzuri inayofanya.
Dk. Shein
aliyasema hayo katika sherehe ya kukabidhi Tunzo kwa wanamichezo bora wa mwaka
2013, huko katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar-es-Salaam sherehe ambazo
zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Katika hotuba
yake Dk. Shein alisema kuwa bila ya kuwepo ushirikiano na maelewano mazuri,
uendeshaji wa shughuli za michezo utakuwa na changamoto nyingi na kueleza kuwa michezo
imekwua ikiwaunganisha Watanzania kwa lengo la kuendelea kuwa wamoja, wenye
mshikamano na kusahau tofauti zao ziliopo zikiwemo za kisiasa, dini, kabila ama
rangi.
Dk. Shein ambaye
ana rikodi nzuri katika anga za michezo enzi zake, aliendelea kueleza kuwa michezo
hujenga udugu, huimarisha mapenzi baina ya wanachama, wapenzi, wachezaji na
washabiki wa timu mbali mbali na kueleza kuwa hivi sasa kila mmoja anashuhudia kuwa
michezo ni chem chem ya furaha na si kuleta maudhi kwenye jamii.
Alisema kuwa
michezo ina umuhimu mkubwa katika historia ya Tanzania ambapo imeweza kusaidia
sana kuwaunganisha Watanzania katika nyakati mbali mbali akitolea mfano chama
cha ASP ambacho kinatokana na chama cha African Association na Shirazi
Association ambapo African Association chimbuko lake ni vuguvugu la michezo.
Dk. Shein ambaye
alikubali ombi la TASWA kuwa mlezi, alieleza kuwa inafurahisha kuona kuwa chama
hicho kinathamini umuhimu wa michezo na tangu kuundwa kwake zaidi ya miaka 40
iliyopita imefanya mambo mengi ya msingi katika kukuza vipaji vya wanamichezo
nchini na waandishi wa habari za
michezo.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa wakati umefika wa kuifanya Tanzania itajike katika michezo mbali
mbali katika ngazi za Kikanda na Kimataifa kwani katika mashindano ya michezo
katika ngazi za Kimataifa bado Tanzania haifanyi vizuri.
Alisema kuwa
jitihada za ziada katika kuimarisha mpira wa miguu, riadha, netiboli na michezo
mengine yote inayopendwa na Watanzania sambamba na kuwandaa wanamichezo wenye
kuweza kufikia kiwango cha mabingwa wa zamani mfano Filbert Bayi, Suleiman
Nyambui na wengineo.
Kwa maelezo ya
Dk. Shein kinachotakiwa hivi sasa ni kuimarisha uongozi na utendaji wa vyama na
vilabu vya michezo ili muda mwingi utumike katika kuendeleza vipaji vya michezo
badala ya hali iliopo hivi sasa ya kulaumiana.
"Lawama
zisizokuwa na msingi hazijengi bali hubomoa hivyo tunahitaji kushirikiana na
kujenga ari kwa pamoja",alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa wakati umefika kwa vyama au vilabu vya michezo kuanzisha shule au
vituo vya michezo kama ilivyokuwa ikifanya hapo zamani ili kukuza vipaji vya
vijana mapema kama inavyofanyika katika nchi za nje.
Alisema kuwa
kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kunawafanya vijana walio wengi
kuutumia muda mwingi sana kwa kutimiza michezo badala ya kushiriki katika
michezo. " Utawakuta vijana wanawajua wachezaji wa timu za Ulaya bila ya
kusoma popote lakini majina ya walimu wa skuli yake hayafahamu",alisema
Dk. Shein.
Alisema kuwa
Serikali zote mbili zimeweka mkazo maalum katika kurejesha michezo mashuleni
kwa kutambua kuwa maskuli ndio chem-cehm ya kutoa wanamichezo wenye vipaji.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Utalii na Michezo
wa Tanzania Bara Mhe. Dk. Fenella Mkangara alisema kuwa jitihada za pamoja
zinahitajika katika kuimarisha sekta ya michezo na kusisitiza haja ya kuwaenzi
wanamichezo kuwa ni la kila mtu.
Mapema uongozi wa
TASWA ulitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kukubali mwaliko huo ambapo pia,
ulieleza vigezo vilivyotumika katika kuwapata watunukiwa tunzo hao.
Akitoa wasfu wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye ametunikiwa tunzo
ya heshima ya wanamichezo Bora, Mwandishi wa Habari Mkongwe Salim Said Salim
alisema kuwa anamfahamu Mzee Karume kuwa mwanamichezo katika michezo ya dhuna,
karata, bao pamoja na mpira wa miguu.
Alisema kuwa
Marehemu hakuwa akifuatilia soka la visiwani peke yake bali alikuwa mpenzi
mkubwa wa Yanga na klabu ya Liverpool ya Uiengereza ambapo baada ya kujenga
uwanja wa Amani Mzee Karume alitoa Shilingi 200,000 ambapo kwa thamani ya sasa
ni Tsh. Milioni 60 kwa ajili ya kujenga klabu ya Yanga iliyopo Jangwani na
baadae akaisaidia Simba ili nayo ijenge jengo la klabu yake hapo Msimbazi.
Katika sherehe
hizo Dk. Shein alimtunukia tunzo hiyo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambayo
ilipokelewa na Mjane wake Bibi Fatma Karume ambaye baada ya kupokea tunzo hiyo
alitoa shukurani kwa waandaaji na kutoa wito wa kuimarisha michezo sambamba na
kusisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi.
Mzee Karume ameshinda tuzo maalum
ya watu waliotoa mchango mkubwa kwenye michezo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha
Simba na Yanga kumiliki majengo yao. Aidha, Dk. Shein alitoa tunzo kwa Mwanamichezo
bora wa Tanzania wa Mwaka 2013 Sherida Bonifas.
Wengine waliopata tunzo hizo ni kiungo wa Azam FC, Erasto Nyoni ameshinda
tunzo ya Mwanasoka Bora ya Chama cha Waaandishi wa Habari Tanzania (TASWA),
wakati Sheridah Boniface amekuwa mwanamichezo bora wa mwaka 2013/2014.
Nyoni aliyeibukia Vital`o ya
Burundi, ameshinda tunzo baada ya kuwangusha Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub
`Cannavaro` na mshambuliaji wa Simba Elias Maguli.
Nae mshambuliaji wa TP Mazembe ya
DRC, Mbwana Samatta ameshinda tuzo ya mwanamichezo bora anayecheza nje, wakati
Kipre Tchetche wa Ivory Coast amewashinda Mbuyu Twite (Rwanda) na Amis Tambwe
wa Burundi katika tuzo ya mwanasoka wa kigeni nchini.
Sheridah ameshinda tuzo tatu,
mwanamichezo bora wa jumla, mwanasoka bora wa kike na mwanamichezo bora
chipukizi, Novatus Emmanuel ameshinda katika Tenis ya walemavu wanaume na kwa
wanawake Rehema Said, Magongo ameshinda Joan Wilson na Kidawa Suleiman, Wavu
wameshinda Teddy Mgwao na Kevin Peter, Riadha ni Alphonce Felix na Zakia
Mrisho.
Katika kikapu Ahmed Liyamaiga,
wakati netiboli ni Dolita Mbunda, Kuogelea mshindi ni Hilal Hila na Catherine
Masoon, mshindi wa judo, Godfrey Mtao na Grace Mhanga.
Tenisi Omar Sule na Rehema
Athumani, ngumi za kulipwa ni Francis Cheka, ridhaa ni Suleimani Kidunda,
katika mshindi wa gofu ni Hassan Kadio wakati kwa ridhaa Nuru Mollel, Baiskeli
Sofia na Richard Laizer.
Mpira wa mikono ni Ahmed Saleh na
Veronica Mapunda ambapo Olimpiki maalumu ni Raphael Kalukula na Brandina Brasi.
Viongozi mbali mbali walihudhuria
katika hafla hiyo akiwemo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa
Tanzania Bara Dk. Fenella Mkangara, Kaimu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo wa Zanzibar Mhe. Abdillah Jihad Hassan,Mkuu wa Mkoa wa Dar-es Salam Mhe. Said Meck Sadik, pamoja na viongozi wa
michezo mbali mvali na waandishi wa habari kutoka pembe zote za Tanzania.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment