Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa
Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema uteuzi wa Assad ulianza Novemba 5,
mwaka huu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa
Assad ataapishwa leo saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi wake, Assad
alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
anachukua nafasi ya Ludovick Utouh, ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi
wa umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye
weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana shahada
ya uzamivu wa uhasibu (PhD in Accounting)
kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na shahada ya uzamivu
katika udhibiti wa fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland
mwaka 1991.
Pia ana stashahada ya kitaaluma
ya uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na shahada ya biashara
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1988.
Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad ana
uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi.
Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na
Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007
- 2014); ni Rais na mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012; na ni
mjumbe wa bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika uteuzi huo, Rais Kikwete alisema ana
imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu wake utamwezesha kutekeleza vyema
majukumu ya nafasi hiyo muhimu katika utawala bora.
No comments:
Post a Comment