Rais wa Zanzibar na Mqwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Nchini Tanzania Dr.Jama Gulaid alipofika Ikulu Mjini Unguja akiwa na ujumbe aliofuatana nao leo
Rais wa Zanzibar na Mqwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Nchini Tanzania Dr.Jama Gulaid alipofika Ikulu Mjini Unguja leo.[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
12.12.2014

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Watoto ulimwenguni (UNICEF) limepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kupiga vita udhalilishaji wa watoto pamoja na mafanikio
yaliopatikana katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto hapa
nchini.
Pongezi hizo zimetolewa
leo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto
Ulimwenguni (UNICEF) nchini Tanzania
Mhe. Jama Gulaid wakati alipofanya mazunbgumzo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo
yake Mwakilishi huyo wa UNICEF hapa nchini alieleza kuwa Shirika hilo
limevutiwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya
Ungozi wa Dk. Shein kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto
na kuahidi kuendelea kuziunga mkono juhudi hizo.
Alisema kuwa
mafanikio makubwa yameweza kupatikanwa hapa nchini ambapo hivi sasa watoto
wengi wamekuwa wakipata haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na fursa ya kujiunga
skuli na kupata haki yao ya elimu pamoja na huduma za afya na nyenginezo.
Aidha, Mhe.
Gulaid alitumia fursa hiyo kuwapongeza wazazi kwa juhudi zao hizo za kuwapatia
elimu watoto kwa kushirikiana na serikali yao katika kuwatunza na kuwalinda
watoto pamoja na kupongeza juhudi za serikali katika kupunguza vifo vya akina
mama na watoto vilivyotokana na maradhi mbali mbali yakiwemo Malaria.
“Leo vifo vya
watoto wachanga vimepungua, watoto wengi zaidi wanakwenda skuli, watoto
wanahifadhiwa zaidi na kupatiwa msaada wa kisheria pale unapohitajika..hongera
sana pamoja na Wazanzibari wote kwa ujumla”,alisema Gulaid.
Mhe. Gulaid ambaye
alifuatana na watendaji wa Shirika hilo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar alisema
kuwa uzinduzi wa Kampeni ya kupiga vita ukatili na udhalilishaji wa wanawake na
watoto uliofanywa hivi karibuni na Dk. Shein umedhihirisha wazi jinsi Serikali
inavyowajali watoto wka kuamini kwamba suala zima la udhalilishaji kwa watoto
litapungua ama kuondoshwa kabisa.
Pamoja na hayo,
Mwakilishi huyo alieleza kuwa katika kutekeleza wasia aliowapa Mhe. Rais wakati
walipokutana mwaka jana kwa kuangalia
uwezekano wa kuwawezesha wananchi, alieleza kuwa tayari wameshakushanya
rasilimali za kutosha katika kusaidia afya ya mama na mtoto, elimu pamoja na uhifadhi
wa mtoto.
Alieleza kuwa
katika kuunga mkono katika maeneo hayo makubwa matatu tayari shirika lake
limeshakusanya rasilimali za kutosha ambapo kwa upande wa afya ya mama na mtoto
shirika hilo limeahidi Dola za Kimarekani milioni 12 na Dola milioni 6.5 kwa
elimu na Dola 15 katika kupambana na maambukizo ya virusi vya ukimwi.
Aidha, Mwakilishi
huyo alisema kuwa katika kuwajengea watendaji uwezo Shirika hilo litaimarisha
kituo cha Afya cha Kivunge ili kipate uwezo wa kutoa huduma bora kwa watu zaidi
ya laki mbli wanaoishi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kwa upande wa sekta ya elimu
aliwataka wazazi kuwaandikisha watoto wao skuli kwa wakati.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake alieleza kuwa UNICEF ni miongoni mwa mashirika ya Umoja wa Mataifa
ambalo limekuwa likiiunga mkono Zanzibar kwa kipindi kirefu na kulipongeza kwa
misaada yake mbali mbali kwa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kwa dhati kupunguza ama
kuondosha kabisa udhalilishaji wa wanawake na watoto na uzinduzi wa Kampeni ya
kupiga vita masuala hayo uatasaidia kwa kiasi kikubwa.
Aidha, Dk. Shein
ameeleza kufarajika kwake na Jumuiya za Kimataifa kuunga mkono Kampeni
hiyo na kueleza kuwa kazi kubwa iliyopo
mbele ni kuielimisha jamii kwani wengi wanaofanya vitendo hivyo huwa katika
familia.
Dk. Shein
alisisitiza kuwa Serikali imeamua kuimarisha jitihada zake katika kufanya
utafiti baina ya nyumba na nyumba ili kuweza kupata takwimu za uhakika.
Aidha, Dk. Shein
amepongeza azma ya Shirika hilo la kuwaongezea uwezo watendaji wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar pamoja na kusaidia fedha katika kuendeleza huduma za afya ya
mama na mtoto, elimu pamoja na uhifadhi wa mtoto.
Dk. Shein
alieleza mafanikio yaliopatika hapa
Zanzibar katika sekta ya afya pamoja na sekta ya elimu na kueleza kuwa hivi
sasa si zaidi ya kilomita tano tayari kumekwua na kituo cha afya ambapo
changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni uhaba wa dawa.
Kwa upande wa
sekta ya elimu alisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake husika imekuwa
ikifanya jitihada katika kuhakikisha watoto waliofika umri wa kuandikishwa
skuli wanapata fursa hiyo na kueleza juhudi zinazofnywa katika kuimarisha
miundombinu ya elimu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment