Na Haji Nassor, Pemba
Waziri wa Biashara, Viwanda na
Masoko Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazuri, ameitaka jamii kuacha dhana potofu ya
kuwaona watu wenye ulemavu kama mzigo, wakikumbuka kuwa huo ni mtihani kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Alisema jamii sasa imekuwa
ikichupa mipaka na kujilaumu na wengine kuona haya hata kuwatoa nje mtoto
mwenye ulemavu na kusahau kwamba hakuna alieomba kuzaliwa akiwa hivyo.
Alitoa kauli hiyo jana uwanja
wa Tenis mjini Chake Chake Pemba, kwenye maadhimisho ya siku ya watu wenye
ulemavu duniani, ambapo kitaifa kwa Zanzibar yalifanyika kisiwani humo.
Alisema sio sahihi kwamba watu
wenye ulemavu hawana mchango wowote kwenye jamii, ambapo dhana hiyo husambazwa
na makundi ya wachache ambao hawana ubinaadamu.
Alisema ipo mifano hai ndani ya
serikali na hata taasisi binfasi, kwamba watu wenye ulemavu wamefanikisha mambo
makubwa na kufuta majina wanayopewa kwamba ni mzigo kwenye jamii.
“Mimi siamini kwamba watu wenye
ulamvu ni mzigo kwenye jamii, maana hata kwenye kampuni yangu, yuko mlemavu
ambae anafanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa, sasa wanaosema ni mizigo hao
wamepitwa na wakati,” alisema.
Katika hatua nyengine waziri
huyo alisema serikali imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira mazuri ili kuona watu
wenye ulemavu wanapata haki na fursa sawa.
Alisema hata uwepo wa sheria
namba 9 ya mwaka 2006 ni miongoni mwa hatua thabiti ambayo kwa sasa imeweka
mazingira imara sambamba na kuwapatia vifaa.
Akisoma risala ya watu wenye
ulemavu wa mikoa mitano ya Zanzibar, Msataafu wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu (UWZ)
Atie Suleiman, alisema watu wenye ulemavu wamekuwa mara nne ya wananchi
wanaokumbwa na majanga kuliko wengine wasiokuwa na ulemavu.
“Lazima serikali ituandalie
kutupa mazingira mazuri, maana yanapotokezea majanga na mafuriko sisi
huathirika mara nne kuliko wengine,” alisema.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa
na maandamano yalioanza ofisi za Zantel mjini Chake Cake na kupokelewa na
waziri huyo.
Kuna watu bilioni moja
wanaoishi na ulemavu duniani na kwanza watu wenye ulemavu wamefikia 16,533.
No comments:
Post a Comment