Habiba Zarali na Abdi
Suleiman,Pemba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej, amewataka wananchi kisiwani
Pemba, kusirikiana katika kupiga vita ongezeko la maambukizi mapya ya virusi
vya UKIMWI.
Alisema mashirikiano kati ya
jamii nzima yatasaidia kupunguza maambukizi mapya ya visuri vya UKIMWI.
Aliyasema hayo wakati
akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho, katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani,
yaliyofanyika Machomanne mkoa wa kusini Pemba.
Alisema mashirikiano hayo
ikiwemo kuwafichua wahalifu wa ubakaji,kupima kwa hiari na kutumia dawa kwa
walioathirika, kutaleta mafanikio makubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha alisema kusini kwa bara
la Afrika zipo nchi ambazo maambuziki yake yako katika silimia 5 hadi 10 ambapo
hali ni ya kutisha.
Alisema Zanzibar kwa utafiti wa
2012 mambukizi mapya yalikuwa ni asilimia 0.6 ambapo hadi sasa yamefikia
asilimia moja hali ambayo inatisha ikilinganishwa na idadi ya wananchi wake.
Alisema maambukizi ya ugonjwa
wa UKIMWI bado yapo katika visiwa vya Zanzibar hivyo ni wajibu kila mmoja
kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha anayazuia yasienee.
Akizungumzia vituo vya ushauri
nasaha, alisema Zanzibar kuna vituo vya kutoa ushauri nasaha na huduma za mama
wajawazito 156, kutoka 137 kwa mwaka 2012 ambavo vinasaidia kuhakikisha
maambukizi yanapungua.
Aidha aliwataka akina mama waliobainika
kuwa na virusi vya UKIMWI kuhudhuria kliniki mapema kwani ili kuondoa uwezekano
wa mtoto kuzaliwa na maambukizi.
Aidha aliwasihi wananchi
kuachana na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI badala yake
wapewe mashirikiano katika kila hali kwani nao wana haki sawa na wengine.
Alilaani vikali vitendo vya
udhalilishaji wa watoto, ikiwemo ubakaji na kulawitiwa na kuitaka jamii
kutokuwafumbia mamcho wanaohusika.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,
Mwanajuma Majid Abdalla, aliwataka wananchi kupima afya zao ili kuishi kwa
furaha na wale watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza kutumia dawa mapema.
Alisema starehe ni miongoni mwa
vichocheo vya kupata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI hivyo kila mmoja awe
makini juu ya suala hilo.
Alisikitishwa na vitendo vya
udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo na
ustawishaji wao.
Akisoma risala ya Jumuiya ya Watu
Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Zanzibar (ZAPHA+), Katibu wa jumuiya hiyo, Saade
Saaduni, aliishukuru serikali na wadau kwa
jinsi wanavyowajali na kuwathamini watu wanaoishi na VVU na UKIMWI.
Walisema watu wanaoishi na VVU na
UKIMWI wamekuwa wakishiriki katika programu mbalimbali za utoaji wa elimu ya UKIMWI
kwa jamii, ikiwemo uhamasishaji wa watu kupima afya zao.
Aliishauri serikali kufikiria
kuanzisha mfuko maaluma wa HIV, kuangalia uwezekano wa kurudisha misaada ya chakula
kwa watu wanaoishi na VVU hasa akinamama wajawazito na watoto wanaotumia dawa
za ARVs na walio katika mazingira magumu.
Wadau wa masuala ya mapambano
ya UKIMWI Zanzibar, ABCZ walisema kuwepo mipango mizuri yenye kutekelezeka kutasaidia
kutokomeza unyanyapaa na vifo kwa watu wanaoishi na UKIMWI.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya
Ukimwi Zanzibar, Prof. Saleh Idris Mohammed, aliiomba serikali kuongeza fedha
katika kukabiliana na mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.
No comments:
Post a Comment