Na Augusta Njoji, Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Ndani,
Mathias Chikawe, amelitaka jeshi la polisi kupanga mikakati thabiti kuhakikisha
amani na utulivu uliopo unaendelea kuimarishwa hasa wakati wa kampeni na
upigaji kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa.
Kauli hiyo aliitoa jana
mjini hapa alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa wakuu wa jeshi
la polisi nchini ambao umefadhiliwa na benki ya NMB.
"Kwa mwaka huu nchi
yetu ina matukio mawili makubwa ya kihistoria na uzoefu unaonesha matukio ya
upigaji kura na chaguzi mbalimbali mara nyingi huwa yanaambatana na vitendo vya
uvunjifu wa amani ikiwemo vurugu, uharibifu wa mali na wakati mwingine
husababisha vifo,” alisema.
Hata hivyo,
alitahadharisha kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa kimataifa na ugaidi na
kusema endapo haitadhibitiwa mapema inaweza kujipenyeza katika sekta mbalimbali
ikiwemo kufadhili watafuta uongozi.
Alisema watu hao
wanatafuta uongozi kwa kutumia fedha zao ili kujiwekea kinga na kujenga misingi
ya kuendeleza uhalifu wao, hali inayohatarisha utawala wa sheria, mfumo wa
demokrasia na upatikanaji wa haki nchini.
"Jeshi hili
naliaagiza kutovumilia watumishi wa aina hiyo na lisisite kuwachukulia hatua za
kinidhamu na kisheria watumishi watakaojiingiza katika ushirikiano wa aina hiyo
ambao unahatarisha amani na usalama wa nchi,"alisema.
Akizungumzaia kuhusu
kuibuka makundi ya kihalifu kama Panya road, Waziri huyo alisema hali hiyo
haikubaliki na kulitaka jeshi hilo kutimiza wajibu badala ya kusubiri matukio
yatokee.
"Wananchi wa Dar es
Salaam wanahoji inakuwaje baada ya taharuki ya Panya road jeshi la polisi
linakamata watu zaidi ya 1,200? Je jeshi la polisi lilikuwa linawafahamu kabla?
Wananchi wanalituhumu jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam kuwa baada
ya kuwakamata vijana wengi limefanya mradi kwa kauli kuwa kuingia bure kutoka
kwa pesa,"alisema.
Alisema iwapo malalamiko
hayo ni ya kweli basi baadhi ya askari wasiowaaminifu wametumia fursa hiyo
kujinufaisha na kuwanyanyasa wananchi na kuagiza hatua stahiki zichukuliwe
endapo ikithibitika kuna ukiukwaji wa maadili mema ya jeshi la polisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Polisi, IGP, Ernest Mangu, alisema jeshi linaweka mkakati kwa kushirikiana na vyama
vya siasa, Msajili wa Vyama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kudhibiti matukio
ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao na zoezi la upigaji kura ya
maoni kwa ajili ya upatikanaji wa katiba.
Aidha alisema takwimu za
uhalifu wa jinai za mwaka 2014 zinaonesha kushuka kwa asilimia 5.7 ikilinganishwa
na asilimia 1.1 kwa mwaka 2013 na jeshi hilo limetenga shilingi milioni 500 kwa
ajili ya kuwazawadia wananchi watakaotoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa
silaha, risasi na miripuko isiyo halali.
No comments:
Post a Comment